BANDA AFURAHIA MCHEZO WAKE WA MWANZO WA LIGI KUU NA KLABU YAKE MPYA

Mshambuliaji mpya mwenye nguvu na uwezo mkubwa wa kukimbia na mpira wa Jang’ombe Boys amesema kwake leo ni usiku wa furaha sana, kutokana na kwamba panapo majaaliwa kesho itakuwa ndio siku yake ya mwanzo kuitumikia klabu yake mpya ya Jang’ombe Boys katika ligi kuu ya Zanzibar.


Mshambuliaji Hassan Seif 'Banda'
akiwa pamoja na Rais wa Jang'ombe
Ali Othman 'Kibichwa'

Akihojiwa mbele ya mtandao huu, mshambuliaji huyo Hassan Seif (Banda) amesema endapo mwalimu akimpa nafasi ya kucheza katika mchezo wa kesho dhidi ya maafande wa KMKM, Banda amesema atakuwa ni mwenye furaha sana.

“Kiukweli baada ya mazoezi takriban ya mwezi mzima, basi sina budi kusema niko vizuri kiafya na kila kitu kinachohitajika katika mchezo, jambo ambalo linanifanya niwe na furaha kwa sababu nitapata nafasi ya kuitumikia timu yangu mpya ambayo nimechagua kuitumikia kwa msimu huu wa 2017/2018.

“Kilichonivutia kwa timu hii ni mengi sana, ikiwemo washabiki wake wastaarabu na wenye moyo na timu yao kwa hali zote, viongozi wake ni viongozi hasa katika mpira, timu ina ubunifu wa hali ya juu katika masuali mazima ya kutafuta mbinu za kukuza mpira nchini, hivyo nawashukuru wadau wote wa timu kwa kunipa nafasi kuitumikia timu hii, na mimi kwa upande wangu endapo kesho mwalimu ataniruhusu niwe miongoni mwa wataocheza mchezo huu, naahidi kuwafurahisha wana Jang’ombe Boys sambamba na kujifurahisha mimi mwenyewe wakati nikiwaona wao wakiwa wamefurahi kwa kazi nitakayowafanyia na nitafurahi zaidi nikifunga goli katika mchezo wa kesho" Alimalizia Banda.


Banda ni miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa msimu huu, akitokea timu jirani na hasimu wa Jang’ombe boys timu ya Taifa ya Jang’ombe.

Maoni