Licha ya kutoka sare ya goli 1-1 katika mchezo wa ligi kuu ya Zanzibar iliyoanza hapo jana katika kiwanja cha Amani Zanzibar, makocha wote wawili wa timu ya Jang'ombe Boys wamefurahishwa na viwango vilivyoonyeshwa na wachezaji wao katika mchezo dhidi ya KMKM.
Kikosi cha Jang'ombe Boys, kilichoanza na KMKM
Akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa Amani mara baada ya pambano hilo kumalizika, kocha msaidizi wa Jang' ombe Boys Issa Othman 'Amasha' alisema kwamba amefurahishwa na viwango vya wachezaji na kama si kikosi chake kuathiriwa na majeruhi basi ushindi kwa timu yake usingezuilika.
"Tumecheza na timu ya KMKM, timu ambayo inaonekana ilijipanga zaidi kwa mchezo huu, kwa sababu ukifuatilia utagundua kwamba timu yao ilikuwa kambini wiki moja ama mbili kisiwani pemba kwa ajili ya mechi hii, kwa matokeo haya siwezi kutoa lawama kwa vijana wangu kwa sababu wamejituma sana.
Akijibu suali la mwandishi wa Star TV Amasha amesema ni kweli timu ilizidiwa katika sehemu ya kiungo lakini, hakukuwa na jinsi zaidi ya kuwaelekeza viungo waliomo ndani kutokana na wachezaji wetu kwa nafasi hio walikuwa na majeraha.
"Middle Field' (Viungo) wetu kweli walichoka, walikufa lakini hatukuwa na namna nyengine ya kufanya, kwa sababu Abdi Kassim na 'Chidi' (Rashid Mohammed), wote wanaumwa (Juma Ali Mohammed aliumwa palepale kiwanjani).
"Mimi nasema mchezo ulikuwa mzuri, kwa sababu timu zote mbili zilicheza kwa kujituma, kushinda, kushindwa na kutoka 'draw' yote hayo ni matokeo ya mchezo, timu yangu sina wasiwasi nayo ndio kwanza ligi inaanza, na nawaambia washabiki wa timu yetu Jang'ombe Boys watulie na nawaahidi tunacheza nane bora na baadae kuwa mabingwa, hivyo washabiki watulie na waendelee kuisapoti timu yao" alimalizia kocha Amasha.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa timu hiyo Said Kwimbi ameshukuru kwa kupata matokeo hayo katika mchezo wake wa kwanza wa ligi kuu, na amefurahishwa na baadhi ya wachezaji jinsi walivyoojesha viwango vya hali ya juu.
"Tumetoka sare ya goli 1-1, si matokeo mabaya ingawa si matokeo yetu, kwa sababu tulitakiwa tushinde na niseme hapa nimepata pa kuanzia ili kukitengeneza kikosi vizuri zaidi ili kushinda katika michezo ijayo ya ligi kuu, kiujumla wachezaji wamejituma vyakutosha" alisema Kocha kwimbi.

Maoni
Chapisha Maoni