Hatimae pazia la ligi kuu Zanzibar kufunguliwa hapo kesho
tarehe 03 Oktoba, ambapo mapema saa nane za mchana kutakuwa na mchezo kati ya
maafande wa vikosi vya JKU na Mafunzo na Jang’ombe Boys FC tutachuana na KMKM
saa 10.00 alasiri.
Na: Mwandishi wetu.
Katika mchezo huo kati yetu na KMKM mshambuliaji wetu
machachari kwa kuzifumania nyavu za timu pinzani, Khamis Mussa Makame (Rais),
ameendelea kutoa vitisho kwa vilabu vinavyoshiriki ligi hio kwa kuwa anaamini
kwa sasa ameimarika zaidi hivyo yuko tayari kwa mchezo na timu yeyote wakati
wowote, na kuzidisha kwamba timu yeyote itakayoingia uwanjani ikiwa mwalimu
atampanga basi wategemee kupokea kichapo kutoka kwake.
Mshambuliaji mahiri wa Jang'ombe Boys
Khamis Mussa 'Rais'
“Mimi binafsi yangu niko tayari kwa mchezo wa kesho na
michezo yote ya ligi kuu, kama nilivyowaliza KMKM msimu uliopita kwa goli langu moja
na jengine kufungwa na mwenzangu ‘Chinga’, basi niseme kesho 'Insha Allah' nitaweka nyavuni zaidi
ya goli moja, na hata washambuliaji wenzangu naamini wanaweza kufunga magoli katika mchezo huo, nasema hivi kwa sababu niseme niko sawa kwa kila kitu, pia timu
imesajili wachezaji wenye kuleta hamasa zaidi ya kimchezo sambamba na
kuengezeka kwa mwalimu Saidi Kwimbi katika benchi letu la ufundi ni dhahiri
hakuna wa kunizuia nisifunge” Alisema Rais.
Katika hatua nyengine Rais amewatoa hofu washabiki wa Jang’ombe
Boys juu ya mchezo huo kwa kusema kwamba, anafahamu kwamba mchezo wa mpira ni
mchezo wa ushindani, lakini amewaomba washabiki wasiwe na shaka.
“Nitoe wito kwa washabiki waje kwa wingi sana kiwanjani, ili kuangalia timu yao na kuniangalia mimi jinsi nitakavotupia magoli langoni kwa
KMKM na kuwafanya waogelee nyasi za uwanja wa Amani kwa huzuni na machungu
nitakayowapa hio kesho, hivyo nawaomba washabiki waache wasiwasi waje kwa
furaha, kwa kuwa nipo vizuri na timu kiujumla wake imeimarika Zaidi” alimalizia
Rais.
Rais aliyasema hayo baada ya mazoezi ya mwisho katika
kiwanja cha mazoezi kabla ya mchezo huo wa kesho wakati alipohojiwa na
mwandishi wa mtandao huu.
TUNAIOMBEA TIMU YETU USHINDI MNONO.

Maoni
Chapisha Maoni