Nahodha wa timu ya
Jang’ombe Boys FC Ibrahim Mohammed (Sangula) amesema timu yake iko vizuri na
hawana wasiwasi juu ya mchezo wao wa kesho wa ligi kuu ya Zanzibar dhidi ya
Mabaharia weusi (Black Sailors), Sangula ambae ni beki kisiki wa timu hio
aliyasema hayo jioni ya leo baada ya kufunga mazoezi kwa ajili ya mchezo huo.
Akizungumza na
mtandao huu Sangula amewatoa khofu washabiki na wadau wa Jang’ombe Boys na kuwaahidi
kwa niaba ya kikosi kitakachopngwa kesho, kwamba washabiki wasubirie kuupokea
ushindi mnono.
Ibrahim Mohammed 'Sangula'
“Tumefanya mazoezi
kwa muda wa wiki mbili, mazoezi yalikuwa mazuri wachezaji tumehudhuria mazoezi
vizuri, tumejituma kwa pamoja, morali ya wachezaji wote imepanda kwa kiwango
kikubwa na kizuri na sasa tuko tayari kuwazamisha mabaharia weusi (Black
Sailor).
“Washabiki waondoe
hofu kabisa juu ya matokeo ya mchezo huu, kwani kwa niaba ya wachezaji wenzangu
nikiwa kama nahodha wa timu hii, sioni sababu ya kushindwa katika mchezo huu
kinyume chake tutajitahidi na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tunarudi tukiwa na
pointi tatu.
“Mashabiki waje kwa
wingi sana kiwanjani kwa sababu ujio wao ni muhimu sana, kwani sisi wachezaji
tunaposikia sauti zao na kuona zile bendera za timu yetu sambamba na
vipeperushi vyengine, huwa morali yetu inaengezeka na kuwa na hamu ya kufanya
vizuri ili kuwaridhisha wao washabiki, ka sababu raha ya mpira ni washabiki na
unapofanya vizuri ndio washabiki huengezeka, alisema Sangula.
Kuhusu kutokuepo
Mshambuliaji machachari katika mazoezi ya leo, Sangula amesema kwamba leo
mchezaji huyo amedharurika kutokana na masuala ya kifamilia, lakini usiku huu
anatazamiwa kuingia kambini ili kujumuika na wenzake kwa mchezo huo.
“Kuhusu kutokuepo
Khamis Mussa (Rais) leo hapa mazoezini,
kam kepteni natambua dharura yake ya kifamilia, lakini tutakuwa nae usiku huu
kambini, kwa sababu ni mzima wa afya na amehudhuria mazoezi wiki zote hivyo kukosa
siku ya leo tena kwa dharura za kibinadamu hakuna tatizo, alimalizia Sangula.
Baada ya mazoezi hayo
timu hiyo imeondoka kuelekea kambini ambapo kesho saa 10.00 alaasiri itamenyana
na Black Sailors FC, huo utakuwa mchezo wake wa pili wa ligi kuu ya Zanzibar
ambapo katika mchezo wa awali Jang’ombe Boys ilitoka sare ya goli 1-1 na timu
ya KMKM, goli la Jang’ombe Boys ilifungwa na Khamis Mussa (Rais).
Tunaiombea ushindi mnono timu yetu hapo kesho.

Maoni
Chapisha Maoni