Jang'ombe Boys FC imefikia maamuzi ya kumsimamisha mshambuliaji wake Abdalla Idd Mtumwa maarufu 'Pienaar' kwa kipindi kisichotajwa kufuatia utovu wa nidhamu na kusababisha fujo kati yake,wachezaji wenzake na viongozi wa timu hio.
'Pienaar' ambae alisajiliwa msimu huu akitokea katika timu ya Gulioni inayoshiriki ligi daraja la pili, nyota yake alianza kungara kwa kupendwa na washabiki, wadau na viongozi wa timu hio, baada ya kuonyesha soka safi na mafahamiano mazuri anapocheza na mshambuliaji mwenzake Khamis Mussa 'Rais', lakini hivi majuzi alisababisha mtafaruku katika kiwanja cha Mwanakombo - Mahonda nje ya mji wa Zanzibar ambapo Jang'ombe Boys walifungwa 4-0 na timu ya Mahonda Kidds inayoshiriki ligi daraja la kwanza Taifa katika mchezo wa kirafiki.
Abdalla Idd Mtumwa maarufu 'Pienaar
Akizingumza na mtandao huu Katibu wa Jang'ombe Boys Abdalla Mahfoudh 'Dallas' amesema Peenar amesimamishwa, kutokana na utovu wa adabu alioufanya Mahonda, ili iwe fundisho kwake yeye na wachezaji wengine wowote watakaokuwa na tabia zisizokubalika katika mpira wa miguu.
"Kitendo alichokifanya Pienaar kutoka uwanjani bila ya ruhusa ya walimu na bila ya sababu za msingi huku akiwa anatukana na kushambulia kwa maneno machafu katika timu yetu hii hakikubaliki, na niseme hakijawahi kufanywa na mchezaji yeyote katika historia ya timu hii tangu tunaanzisha timu hadi hapa tulipo.
"Hivyo kwa hatua za awali ili kuonyesha kwamba tumekerwa na hatukufurahishwa na kitendo kile, kwa hatua za awali tumeamuwa tumsimamishe huku tukitafakari hatua zaidi za kinidhamu za kumchukulia, hivyo wadau wote wa Jang'ombe Boys na wapenzi wa mpira tunawapa taarifa hii kwamba mchezaji wetu Abdalla Idd Mtumwa amesimamishwa kuitumikia timu hii mpaka hapo taarifa nyengine ya hatua zaidi ya kinidhamu itakapotangazwa. Alisema Katibu Dallas.
Katika hatua nyengine pia katibu huyo aligusia kwamba katika siku chache zijazo, pia kuna wachezaji wengine wanne ambao nidhamu zao zimeonekana kulega lega huenda na wao wakasimamishwa ama kufungiwa kuchezea timu hiyo kwa kipindi kitakachoelezwa.
Kwa kifupi katika sakata la Pienaar ni kwamba alipewa jukumu la kupiga penalti wakati timu ilipopambana na watoto wa Kocha Bausi yaani Mahonda Kidds, Pienaar alikosa penalti hio ndipo akatoka na hasira huku akidai kwamba ametupiwa lawama na wachezaji wenzake ndipo akaamuwa kutoka kiwanjani huku akitupa matusi na maneno machafu, jitihada za kumtuliza zilifanywa na makocha, vinongozi na hata wachezaji wenzake, lakini Pienaar aliendelea na hadi kuamuwa kutaka kupigana na Nahodha wake Msaidizi, Rashid Moh'd (Chidi Remember), jambo ambalo lilizusha hisia kali juu yake kwa kila aliyekuwepo kiwanjani hapo.

Maoni
Chapisha Maoni