JANG'OMBE BOYS VS SHABA YA KOJANI KUIPAMBA JUMAPILI YA KESHO.



Timu ya Jang'ombe Boys FC ya kisiwani Unguja itapambana na timu ya Shaba SC kutoka kisiwa cha Kojani huko kisiwani Pemba.

Mpambano huo kati ya Shaba FC na Jang'ombe Boys ni maalum kwa kujipima nguvu timu hizo zinazoshiriki ligi kuu Zanzibar, ambapo Shaba wanashirikiri ligi kuu kanda ya Pemba na Jang'ombe Boys wanaoshiriki ligi kuu Unguja.


Mchezo huo umewavutia wapenzi wengi wa mpira wa miguu, kwa kuwa timu ya Shaba ni timu iliyojibebea umaarufu visiwani humu, kutokana na umahiri wake wa kiuchezaji miaka iliyopita, timu hio pia ilifahamika kwa ugumu wake kufungika sambamba na aina ya washabiki wake.

Kwa upande mwengine wadau pia wanahamu na mchezo huu ili kuishuhudia Jang'ombe Boys ambao walisifika msimu uliopita kwa kuonyesha mchezo wa kiufundi, kiustaarabu sambamba na kuwa na wachezaji wenye vipaji na kasi katika kucheza mpira.

Wachezaji wa J.Boys wakipeana mikakati.


Kihistoria, timu hizo zina historia sawa kati yake, ambapo kumbukumbu zinaonyesha timu hizo zimekutana mara moja, na matokeo yakawa sare ya kufungana magoli manne kwa manne, hivyo pia mchezo huu pia utaamua nani mbabe kati ya Jang'ombe FC VS Shaba FC.

Akithibitisha kuwepo kwa mchezo huo Rais wa Jang'ombe Boys FC Ali Othman (Kibichwa), ameuambia mtandao huu kwamba ni kweli Jumapili kesho tarehe 24 Septemba, timu yake itacheza mchezo wa kirafiki na Shaba FC kutoka Kojani Pemba.

Kikosi cha zamani cha Shaba FC.


"Ni kweli timu yetu itacheza mchezo na Shaba ya Kojani Pemba, ili kuipima nguvu timu yetu kwa mara ya tatu kabla ya msimu kuanza hapo tarehe 03 Oktoba, tumeamua kucheza na Shaba kwa sababu tunaamini Shaba ni miongoni mwa timu ngumu Zanzibar, hivyo hapa ndio ile dhana hasa ya kujipima nguvu itapatikana".

"Tumecheza michezo miwili, mmoja tulicheza na Dula Boys ya Jambiani, matokeo yakawa 1-1 na hivi juzi tumecheza na Villa United ambao ulikuwa ni mchezo maridadi kabisa ingawa matokeo yalikuwa tasa, hivyo nawaambia washabiki wa mpira wa miguu Zanzibar waziunge mkono timu zetu, waje washuhudie vipaji vya soka vya hapa nyumbani, na viingilio vya mchezo huo ni rahisi sana, kwa sababu lengo letu ni kuwaburudisha wapenzi wa soka, hivyo tumeweka viingio sh. 1000/- na sh. 2000/- tu" alimalizia Rais huyo wa Jang'ombe Boys.

Hivyo usikose uhondo huo, karibuni nyote


Maoni