JANG'OMBE BOYS WAIYEYUSHA SHABA YA KOJANI.

Timu ya Jang’ombe Boys FC inayoshiriki liki kuu kanda ya Unguja usiku wa leo wameiyayusha timu ya Shaba FC inayoshiriki ligi kuu kanda ya Pemba kwa kuifunga magoli manne bila ya majibu, ni Jangombe Boys walioonekana kuumiliki mpira na kucheza kwa kasi kubwa sana, kujiamini na maelewano sambamba na kupeana pasi za uhakika tangu dakika ya mwanzo wa mchezo, kitendo ambacho kiliwafanya vijana hao wa Kojani Pemba kupoteana, ambapo Jang'ombe Boys iliwachukuwa dakika 19 tu wakaandika goli la kwanza lililofungwa kwa njia ya penalti na mchezaji Suleiman Ali Suleiman (Pichori) aliyetua klabuni hapo akitokea klabu ya Kilimani City yenye makao yake katika Magorofa ya Kilimani Zanzibar.

Katibu Friends of J.Boys, akikabidhi
Cheti cha mchezaji bora wa mechi 
kwa mchezaji Hassan Choum.


Jang’ombe Boys hawakuridhika na goli hilo walionekana kuzidisha kasi Zaidi na dakika tatu baadae mnamo dakika ya 21 Helfini Salum (Fini) aliyesajiliwa kutoka Kilimani City akaiengezea timu yake goli la pili kuunganisha krosi kali ilichongwa na Hassan Chumu (Mbungi).

Shaba walizidi kuelemewa na vijana hawa wa Jang'ombe Boys na dakika ya 33 Mustafa Vuai Hassan (Tafa-Neimar) akaingezea goli Jangombe Boys goli la tatu la kuongoza, goli ambalo lilidumu hadi dakika ya 56 Tafa akawanyanyua tena washabiki wa Jang’ombe Boys kushangiria goli la nne.

Wachezaji wa Jang'ombe Boys wakinyosha 
viungo kabla mchezo wao na Shaba.


Dakika 59 Shaba walionekana wangepata goli baada ya beki kisiki wa Jang’ombe Boys Ali Humudi Bardu (OCD) kuteleza na kuanguka wakati akiburura mpira na mpira ukaingia miguuni mwa mshambuliaji Wa  Shaba, mshambuliaji huyo alipiga shuti kali ya chini, ambapo ni dhahiri kama si umahiri na uhodari wa golikipa nambari moja wa Jang’ombe Boys Hasham Haroun Ruga kuonyesha umahiri wake na kuufuata mpira huo na kuudaka, basi ilikuwa ndio nafasi pekee ya wazi kwa timu ya Shaba kuandika goli la kufutia machozi.

Dakika 72 baadae golikipa wa timu ya Shaba aliyeingia Kipindi cha pili alifuta goli la wazi kwa kuokoa mpira wa kichwa uliopigwa na Hassan Seif Banda aliyesajiliwa kutokea Taifa ya Jang’ombe ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukuwa nafasi ya mshambuliaji mwenzake Abrahman Othman (Chinga) aliyesajiliwa kutokea klabu ya Singida United ya Mkoani Singida, hadi mwisho Jang’ombe Boys FC 4-0 Shaba.

Katika upande mwengine jopo la makocha waliokuwa wakifuatilia mchezo huo wamemchagua Hassan Choum Abdallah kuwa ndiye mchezaji bora wa mechi hio yaani "Man of the Match", ikumbukwe kwamba Hassan Choum alishawahi kutangazwa mchezaji bora na 'FRIENDS OF J. BOYS' na akakabidhiwa cheti maalum pamoja na fedha.


Maoni