WANACHAMA JANG'OMBE BOYS KUINGIA BURE AMANI KUIANGALIA TIMU YAO IKIPAMBANA NA CHUONI FC.


Katika kuhakikisha kwamba timu ya Jang'ombe Boys inawathamini wanachama wake, kuwaleta karibu na timu yao sambamba kuwafanya wafaidi matunda ya uanachama wao, Friends of Jang'ombe Boys wamelipia wanachama wote wa timu hio kuingi bure kutazama moja kwa moja kutoka kiwanja cha Amani wakati timu itakapocheza na Chuoni FC siku ya Jumanne ya tarehe 24 Oktoba mwaka huu.

Hayo yameelezwa katika taarifa iliyowasilishwa katika mtandao huu jana jioni wakati wa akielezea majukumu na malengo ya Friends of Jang'ombe Boys, sehemu ya taarifa hiyo ambayo imetolewa na Katibu wa Friends of Jang' ombe Boys imesema:


Wachezaji wa J. Boys wakionyesha
furaha kwa mashabiki wao

"TAARIFA KWA WANACHAMA WOTE WA JANG'OMBE BOYS.

24/10/2017 SIKU YA JUMAANE KUTAKUWA NA MECHI YA LIGI KUU ZANZIBAR KANDA YA UNGUJA. MECHI HIYO ITACHEZWA SAA KUMI KAMILI ZA JIONI UWANJA WA AMANI MECHI ITAKUWA KATI YA JANG'OMBE NA CHUONI WANACHAMA WOTE WA JANG'OMBE BOYS WATALIPIWA KIINGILIO NA FRIENDS OF BOYS SIKU HIYO JUKWAA LA URUSI KAMA WEWE NI MWANACHAMA WA BOYS TAFADHALI NJOO NA KADI YAKO TU TIKETI UTAIKUTA UKIPATA TAARIFA HII MWAMBIE NA MWEZIO UKIFIKA PIGA CM 0777360176".
Imetolewa na:

Alawi Haidar Foum.
Katibu Friends Of Boys


Mtandao huu pia ulipata nafasi ya kuzungumza na mshika fedha wa Friends of J.Boys ndugu Ali Mohammed juu ya taarifa hio iliyotolewa, nae kwa upande wake aliuthibitishia mtandao huu kwamba ni kweli mpango huo na umesharatibiwa na kupewa baraka na wanakamati wote wa Friends of J. Boys.

"Ni kweli tumekaa wanakamati wote 56 wa Friends of J.Boys tukiongozwa na mwenyekiti wetu Ahmed Mbarouk, na tukatafakari mambo mengi ambayo yana malengo ya kuifanya timu ifike mbali zaidi ya ilipoishia msimu uliopita, ambapo timu iliishia nafasi ya tatu katika msimamo.
"Pamoja na mambo mengine lakini tumeona uungwaji mkono viwanjani na wanachama wetu ni jambo moja muhimu sana na ni jambo la kupewa kipaumbele cha hali ya juu, hivyo pia upande mwengine tukasema lazima tuwe na kitu ambacho kitawafanya wanachama wetu wao ni muhimu hivyo kuna haja ya kuwafanyia kitu waone kwamba tunawapenda na kuthamini michango yao wanayochangia kila mwezi.
"Hivyo tulipounganisha mambo hayo mawili lile la kuwashajihisha wanachama wafike viwanjani kuipa hamasa timu na lile la kuwafanya wanachama waone kwamba timu inawajali, kuwapenda na kuwathamini ndipo tukatoka na azimio ambalo tayari tumeshaliingiza katika utekelezaji, nalo ni kamati yetu ya Friends of J. Boys ingaramie kuwalipia wanachama wote wa timu yetu.
"Hii maana yake nini? kuna maana pana sana hapa, kwanza wanachama tunataka wajihisi wao ndio chachu ya ushindi wa timu, kwa sababu endapo wakifika kiwanjani wakaishangilia timu bila shaka timu itafanya vizuri, pili tunawataka wanachama wetu wasihisi kwamba wao wanagharamikia timu kwa kulipa ada ya uanachama na michango mengineyo bila ya manufaa yeyote, lakini tunataka wahisi kwamba kumbe na wao wanapata mrejesho katika timu, timu nayo inawajali na kuwapenda kwa kuwaingiza kiwanjani bure" Alimalizia Mshika Fedha Ali Mohammed.
Hii ni hatuwa moja nzuri kwa wanachama wa Jang'ombe Boys FC kufaidi matunda ya timu yao kupitia friends of J.Boys, hivyo jambo la msingi kama bado hujachukuwa kadi ya uanachama, basi ni vyema ukachukuwa ili ufaidike na fursa nyenginezo ambazo Friends of J.Boys wameamuwa kuanzisha.



Maoni