MSHAMBULIAJI WA ZANZIBAR HEROES AAHIDI KUENDELEZA REKODI YAKE KUIFUNGA TAIFA YA JANG'OMBE

Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) leo Jumatano tarehe 22/11/2017 inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya Taifa ya Jang’ombe katika mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu kabla ya timu hiyo baadae kusafiri kuelekea jijini Nairobi katika mashindano ya 'Challenge Cup, 2017, pambano litavurumisha mnamo majira ya saa 2:00 za usiku katika uwanja wa Amaan.

Mtandao huu ulifanya mahojiano na mchezaji wa timu ya Taifa ya Zanzibar Khamis Mussa Makame (Rais), ambaye ana historia ya kuifunga Taifa ya Jang'ombe, awapo katika timu yake ya Jangombe boys pindi timu hizo zikikutana na mahojiano yalikuwa hivi:

Suali: Jee unauzungumziaje mchezo wa leo dhidi ya Taifa ya Jangombe wakati mtakapo kutana?

Rais:  Mchezo wa leo nategemea utakuwa mzuri sana na ni matarijio yangu kwamba tutashinda mchezo huu, ili kuwatoa khofu Wazanzibari kutokana na sare ya bao 1-1 tulitoka katika mchezo wa awali.

Suali: Hali ya timu yenu ikoje, kwa sababu tuna taarifa kwamba baadhi ya wachezaji ni wagonjwa hivyo hawataweza kuunga nguvu mchezo huo?

Rais: Kwa sasa mwenzetu Ali Badru ndio kidogo hali yake sio nzuri na kipa pia na yeye anasumbuliwa kidogo, ila tuna wachezaji mbadala wao.

Suali: Umekuwa na kawaida ya kufunga goli kila unapokutana na Taifa ya Jangombe, lakini hili huwa unalifanya pindi ukiwa na timu yako ya Jangombe Boys, jee ukiwa na kikosi cha timu ya Zanzibar Heroes, unadhani unaweza kuendelea na utaratibu huo?

Rais: Ni kweli, na naahidi kurudia hilo endapo nikipewa nafasi na mwalimu, na niseme nina imani kubwa ya kuifungia timu yangu Zanzibar Heroes leo.

Suali: Huoni kwamba kutakuwa na ugumu, kutokana na Taifa ya Jangombe kufanya usajili mkubwa msimu huu zikiwemo nafasi zote sambamba na kuwa na beki imara ambayo haipitiki kirahisi?

Rais: Niseme kwa upande wangu pia nimepevuka zaidi na nimepandisha kiwango zaidi, na kwa jinsi tunavocheza kwa muunganiko mzuri katika timu hii, tunatengenezeana nafasi za kutosha na utulivu uliopo katika timu sioni sababu nisifunge.

Suali: Unawaambiaje washabiki wa Zanzibar, ukiwa na timu ya Taifa ya Zanzibar katika mchezo huu wa leo?

Rais: Washabiki wote wa Zanzibar nawaambia hapa nipo kwa ajili ya Taifa letu, hivyo nawaahidi ushindi katika mchezo huu, pia katika michezo mengine katika mashindano, nawaomba waelekeze dua zao nyingi kwetu ili tuondoke na baraka zao na tukafanye vyema huko katika mashindano.

----Mwisho-------

Maoni