'SANGULA' WA JANG'OMBE BOYS ATOA 'NENO' BAADA YA KUCHAGULIWA TIMU YA TAIFA YA ZANZIBAR 'ZANZIBAR HEROES'

Beki kisiki ambaye pia ni nahodha wa timu ya Jang'ombe Boys Ibrahim Mohammed (Sangula) amefanya mahojiano mafupi na mtandao huu, mtandao ulimtafuta Sangula ili kuthibitisha kama ndiye yeye jina lake lilitajwa katika orodha ya wachezaji 30 yalipotajwa na Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) Hemed Suleiman (Morocco), na kujuwa iwapo ameupokea uteuzi huo na kama ameupokea ameupokea vipi:


Sangula akiwa na waamuzi wakati 
wa mashindano ya 'Rolling Stone' jijini Arusha 
ambapo Wilaya ya Mjini walitwaa kombe hilo 2016.

SWALI: Masikio ya Wazanzibari yamesikia jina lako likitajwa katika orodha ya majina 30 ya wachezaji watakaounda kikosi cha timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) ambacho hapo baadae kitasafiri nchini Kenya ili kushindana katika mashindano ya Kombe la Chalenj, jee vipi unaweza kuuthibitishia mtandao huu kwamba hio ni kweli?                             

SANGULA: Ni kweli jina langu limetajwa katika wachezaji wanaounda timu ya 'Zanzibar Heroes', na niseme sikuwa najuwa kwamba labda ningetajwa siku ile, ila nilianza kupokea simu kutoka kwa wadau na washabiki wangu mbali mbali kunipongeza, kunipa moyo na kunitaka niendelee kukaza buti ili kufika mbali zaidi, kwa hiyo niseme ni kweli nimo katika kikosi hicho cha awali.

SWALI: Jee umeupokeaje uteuzi huo wa wewe kuwemo katika kikosi cha timu hio ya 'Zanzibar Heroes'?.

SANGULA: Kwa kweli nimeupokea kwa furaha na nahisi ni faraja sana kwangu, kwa sababu naamini Zanzibar ina vipaji vingi vya wachezaji ambao wanauwezo zaidi ya mimi, lakini mimi ndiye niliyebahatika kuchaguliwa katika katika kikosi hicho cha watu 30, niseme hizi ndizo miongoni mwa ndoto zangu kwamba siku moja nicheze katika timu ya taifa langu na niipaganie ili niweze kuiletea ushindi.

SWALI: Kwa kuwa unaamini kwamba Zanzibar ina vipaji vingi vya wachezaji, jee! unaamini kwamba unastahili kuchaguliwa katika kikosi hicho na kuacha hao walioachwa?

SANGULA: Kocha 'Morocco' ni kocha mkubwa sana kwa Afrika Mashariki na kati niseme nikocha ambaye habahatishi katika kazi yake na wala hana ubaguzi au mapenzi binafsi, hivyo mwalimu ameangalia kazi yangu ninavyoifanya ninapokuwa kiwanjani na mwisho akatoka na suluhisho la kuniona kwamba nafaa, hivyo niseme mwalimu hakukosea na hili nitalithibitisha kwa vitendo 'In sha Allah'.

SWALI: Jee! Ulishawahi kuchaguliwa katika timu ya Taifa ya Zanzibar kabla ya uteuzi huu?

SANGULA: Kwa timu ya Taifa kubwa ya Zanzibar hii ni mara ya kwanza na ndio mana ninafuraha sana na matumaini mema katika kazi hii, ama kwa timu za vijana nimeshachaguliwa sana hata mwaka juzi kama unakumbuka nilikuemo katika timu iliyoshiriki Mashindano ya 'Rolling Stone'.

SWALI: Mara nyingi nimewahi kukusikia ukisema una ndoto ya kucheza soka la kulipwa nje ya Zanzibar, jee unadhani kuchaguliwa kwako katika kikosi hichi ni njia moja wapo ya kutimiza ndoto yako hio?

SANGULA: Bila ya shaka, hii ni hatua moja ya kufikia kule zilipo ndoto zangu, kwa sababu kuchaguliwa katika timu ya Taifa ya nchi yako ni heshima na pia kunatengeneza 'CV', hivyo naanza kuuona mwangaza wa nuru ya kuimurika ndoto yangu.

SWALI: Kuteuliwa kwako huko ni sawa na kujibebesha dhima kwa Wazanzibari. Jee! unawaahidi nini Wazanzibar, Kocha, viongozi, wadau na washabiki wako wote?

SANGULA: Kwanza niwatoe hofu hao wote uliowataja juu ya uteuzi huu wa wachezaji 30, kikosi nikizuri sana, hivyo kwa kushirikiana na wenzangu sambamba na ridhaa na dua za wadau wote, basi nawaahidi Wazanzibari tutafanya vizuri kwa maslahi mapana ya nchi yetu sambamba na mimi mwenyewe kukitangaza kipaji changu vizuri, na naamini kwa uwezo wa Allah tutafanya vizuri.

SWALI: Unawaambiaje wachezaji wenzako ambao mmechaguliwa katika kikosi hicho?

SANGULA: Kwanza niwapongeze wote waliochaguliwa katika kikosi hicho, pili niwaambie tupiganie kwa pomoja kikosi hicho, kwa sababubu hapa tumelibeba taifa na dhamana ya Wazanzibar wote tumeibeba sisi watu 30, ina maana tunatakiwa tupigane na tupambane kwa maana ya kupambana kwa maana ya kulipigania taifa letu ili kuliletea heshima Zanzibar yetu.

SWALI: Ibrahim, kwa niaba ya timu nzima ya mtandao huu, tunakupongeza kwa kuteuliwa kwako katika kikosi cha timu ya taifa ya Zanzibar, tunakuombea duwa ukaliwakilishe vyema taifa lako ili iwe ndio sababu ya kutimiza ndoto zako na pia tunakushuku kwa wakati wako.

SANGULA:  Ndugu mwandishi kabla sijakuaga niombe angalau dakika 2,3 nitoe shukurani zangu kwa walionizunguka.

Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniumba na kunipa uhai wake na kufikia kuyafanya haya yote yanayoendelea, pili kwa wazazi wangu kwa kunilea katika maadili mema ambapo niseme hicho nikitu kimoja kinachonibeba katika maisha yangu, pia niwashukuru watu wa familia yangu wote wakiwemo ndugu zangu, kaka na dada zangu.

Pia niwashukuru sana wadau wote wa Jang'ombe Boys, kuanzia makocha viongozi na washabiki wote nisiwasahau wadau wote wa Zanzibar kwa sababu nina washabiki mpaka katika timu zenye upinzani na timu yetu.

Niwashukuru Makocha wangu wote waliowahi kunifundisha, Kocha Amasha, Kocha King, Kocha Richkard, Kocha Maha, Kocha Kwimbi, Kocha Teo na wote ambao sikuwaorodhesha hapa.

Mwisho nimshukuru kwa dhati kakaangu Ali Mohammed ambaye amekuwa ni muhimili mkubwa na muhimu sana katika mambo yangu haya ya soka na mengineyo.

Wote nawaambieni sikuchaguliwa timu ya Taifa kwa nguvu na mabavu yangu, bali nimechaguliwa kwa busara na hamasa zetu, hivyo nawaahidi kuendelea kuyafanyia kazi maelekezo yenu yote ambayo mlionipatia na mtakayoendelea kunipatia - Niseme nawapenda na nawathamini sana.

Na naushukuru mtandao huu kwa kwa kunipa fursa hii fupi na nasema ni fursa ya thamani sana, Ahsanteni sana.



---MWISHO---




Maoni