Mshambuliaji mwenye nguvu na mwenye uchu wa kupachika magoli wa timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) Ibrahim Hamadi Hilika (Mbappe) ambaye jana ndiye aliyeizamisha Timu ya Taifa ya Tanzania Bara kwa kufunga goli la pili, amesema ni mafunzo ya Kocha wa kikosi hicho Hemed Suleiman 'Morocco' ndiyo siri pekee ya timu yake "Zanzibar Heroes' kutoka kuongozwa goli 1-0 na Tanzania bara hadi kurejesha na kushinda kwa goli 2-1 katika mashindano ya CECAFA Senior Challenge cup yanayoendelea huko Kenya.
Hilika akishangiria na wachezaji wenzake wa Zanzibar
Heroes baada ya kupachika goli la pili na la ushindi dhidi ya Tanzania Bara
Hilika aliyasema hayo kwa hisia kali wakati akihojiwa na vyombo vya habari kutaka kujuwa ni ipi siri ya ushindi huo dhidi ya Tanzania bara, wakati hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza kinamalizika Tanzania Bara walikuwa wakiongoza kwa goli 1-0, Hilika alikuwa na haya ya kusema.
"Kwanza tunamshukuru Mwalimu wetu (Hemed Suleiman 'Morocco), mwalimu anatufundisha vizuri na anatuhamasisha vuzuri, kwa sababu mwalimu anatwambia kila mmoja binafsi ni mkali kwake, na mwalimu anatupa mafunzo bora na ya msingi ambayo ndiyo yaliyotufanya leo sisi tukafanya vizuri.
"Hivyo tunamshukuru sana kwa sababu tumeingia ndani tukiwa mechi inatuongoza goli 1-0, lakini tulipokuwa vyumbani mwalimu alitwambia tusiwe na wasiwasi mechi tutashinda goli 2 hadi tatu (iwapo wangemsikiliza maagizo yake).
"Na kweli tulimuamini kwa sababu na sisi tunajiamini, hivyo tunamshukuru sana mwalimu kwa kutufanyia hesabu nzuri silizotufanya tupate ushindi siku ya leo" Alisema hilika.
Kwa ushindi huo dhidi ya Tanzania Bara, Zanzibar imekamata usukani wa kundi A kwa kuwa na alama 6 ikifuatiwa na wenyeji Kenya wakiwa na alama 4, huku Tanzania Bara ikikamata nafasi ya 4 nafasi moja juu ya Rwanda ambao ndio wanaoshika mkia wa kundi hilo.
Endapo 'Zanzibar Heroes' itashinda mchezo wake dhidi ya wenyeji Kenya au kupata suluhu ya aina yeyote basi Zanzibar itakuwa imefuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Maoni
Chapisha Maoni