KUNA HAJA YA SERIKALI NA WADAU KUIBORESHEA MASLAHI ZANZIBAR HEROES ILI TUCHUKUWE UBINGWA WA CECAFA 2017

Ni matumaini yangu kwamba Wazanzibar wote waliomo ndani ya visiwa vya Zanzibar na hata wale walio nje ya visiwa vya Zanzibar, wapenda michezo na wasiopenda michezo sote tunaelewa kile kinachoendelea kule nchini Kenya katika mashindano ya CECAFA Senior Cup 2017, kwa kuwa naamini Wazanzibari walio wengi huwa hawako nyuma na hawafanyi mzaha katika jambo zima linalohusu taifa lao, ndio mana imani yangu ikajengeka hivyo na ikiwa kuna Mzanzibari nimemjumuisha kimakosa katika hili basi nasema 'Kum radhi'.



     Na: Ali Mohammed

Katika mashindano hayo ya CECAFA Senior Cup, kuna jumla ya timu 9 zilizogawanywa katika makundi mawili, yaani kundi A na B, kundi A lina timu 5 ambazo ni Kenya, Zanzibar, Rwanda, Libya na Tanzania Bara, na kundi B lina timu 4 ambazo ni Uganda, Burundi, Ethiopia na Sudani ya Kusini.

Msimamo wa Makundi yote mawili ya CECAFA Senior Cup 2017

Timu zote hizo zimeshacheza baadhi ya michezo yake, kuna zilizocheza mchezo mmoja mmoja, kuna zilizocheza michezo miwili, kuna hadi zilizocheza michezo mitatu, pamoja na kutofautiana kimichezo lakini hadi sasa ni Zanzibar Heroes pekee ndio inayoonyesha kitisho na ubabe katika mashindano hayo, kwa sababu, Zanzibar imecheza michezo miwili pekee na imeshajikusanyia alama 6, ambapo amewapita hata waliocheza michezo mitatu katika makundi yote.

Labda unaweza kufikiri makala hii haikupaswa kuandikwa hadi pale wale waliocheza mchezo mmoja na wao wacheze mchezo wa pili kama walivyocheza Zanzibar Heroes michezo miwili, lakini hata makala hii ingesubiri hivyo, jawabu ni kwamba katika timu zilizocheza mchezo mmoja nazo ni za kundi B pekee, hata zishinde michezo yake ya pili, lakini haziwezi kufikisha alama 6, kwa sababu timu hizo ni Uganda na Burundi ambapo Uganda ana alama 1 na Burundi hana alama hata 1, hivyo endapo Uganda akimfunga Burundi atafikisha alama 4 pekee na Burundi ikiwa atamfunga Uganda atakuwa na alama 3 pekee.


Kikosi cha Zanzibar Heroes 2017

Hivyo hadi sasa taa ya kijani (Green light) imeshawaka kuashiria Zanzibar Heroes wana nafasi nzuri ya kutinga hatua ya nusu fainali na baadae  na ya ubingwa kwa msimu huu wa CECAFA Senior Cup 2017, lakini hili halitakuja bila kuboresha mazingira ya vijana wetu, ili wazidishe ari na hamasa ya kufanya vizuri zaidi katika michezo iliyobakia.

Kuna haja Serikali, mamlaka zinazosimamia michezo (ZFA) na wadau wa michezo Zanzibar kuwaboreshea maslahi vijana wetu, kuanzia posho, huduma za ziada, mbali ya zile zinazotolewa na waandaaji wa mashindano hayo, uhakika wa usafiri mzuri wakati wa kurudi tafauti na ule waliokwendea nchini Kenya na ahadi nyengine mbali mbali zitakazokuwa na utekelezaji tena kwa wakati.

Nasema hivi kwa sababu sote tunaelewa kwamba mafanikio hasa hasa katika utendaji wa kazi hayapatikani bila ya juhudi za wafanyakazi (Effort) na msukumo (Motivation), sasa wafanyakazi wetu kwa maana wachezaji na benchi zima la ufundi wameshaonyesha juhudi zao kilichobakia ni msukumo (motivation) wa waajiri wao ili mzigo ufike vyema na kwa wakati.

Tukifanya hivyo naamini vijana watafanya vizuri zaidi ya walivyafanya hivi sasa na sifa na heshima itakayopatikana itakuwa ni yetu sote.




Maoni