WACHEZAJI 'ZANZIBAR HEROES' MSIKHOFISHWE NA KUGIDWA MKOJO NA KUFYONZWA DAMU, PIGENI KAZI NUSU FAINALI MSHINDE NA TUCHUKUWE KOMBE.
Bila ya chembe ya shaka wengi wa Wazanzibari au karibia wote ni mashuhuda wa kile kinachoendelea kule nchini Kenya katika mashindano yanayoendelea ya CECAFA Chalenj Cup, kuanzia mechi ya mwanzo hadi hapa mashindano hayo yalipofikia, ambapo tunasubiria nusu fainali mbili moja ni kati ya Zanzibar Heroes watakaopambana na Uganda na ya pili ni ile kati ya wenyeji Kenya na Burundi.
Lakini ninachotaka kukishuhudisha zaidi hapa si uzuri na haiba ya mashindano wenyewe, na si kuimarika kwa baadhi ya vikosi na kudhoofika kwa baadhi ya vikosi, laa hasha! si hivyo, bali lengo ni kukushuhudisha kile kibweka cha mashindano haya, pale Mawakala wa kupinga utumiaji wa dawa za kuongeza nguvu Michezoni kupitia tawi lao nchini Kenya (World Anti-Doping Agency “WADA”) kuwapima wachezaji wa timu ya Zanzibar Heroes, kibweka hicho cha mashindano kilifanywa baada ya Kenya kushindwa kuifunga Zanzibar Heroes katika mchezo ambao Kenya walipania na kujidhatiti kupata ushindi.
Mawakala hao walifika katika hoteli ya Garden iliyopo Machakos Mjini Kenya, ambapo ndio waliyokua wakikaa kambi timu yetu ya Taifa ya Zanzibar, na maafisa hao walifika kuchukuwa vipimo kwa wachezaji wetu wanne ambao ni Kiungo Mohd Issa “Banka”, Fesal Salum “Fei Toto” na Washambuliaji Ibrahim Hamad Hilika na Suleiman Kassim “Seleembe”.
Lengo la vipimo hivyo vilielezwa kwamba eti wana wasiwasi wachezaji hao huenda ikawa wanatumia dawa za kusisimuwa misuli, kiufupi dawa hizo zinazotuhumiwa kazi yake kuu ni kuwarejeshea nguvu wachezaji pale ambapo wamechoka, hvyo endapo wakitumia dawa hizo huwa wanawazidi wachezaji wa timu pinzani kwa sababu wao huwa hawachoki.
Cha ajabu zaidi ni zile kauli za chini chini za maafasa hao walizoakuwa wakitoa kwamba eti “Mechi tatu mfululizo Zanzibar wanacheza kwa kiwango bora, tena wachezaji wao ndo wale wale kila siku wanaoanza labda abadilike mmoja tu, itakuwa wanatumia dawa za kuongeza nguvu lazima wachunguzwe”.
Kwa kuwa Wazanzibari ni wasikivu na ni watii wa sheria bila shuruti, hatimae vijana na viongozi wao walilipa baraka suala lile na walikubali, wakachukuwa sampuli (Sample) zote za vipimo walivyohitaji vikiwemo choo kidodo (mkojo) na damu, ambavyo hivyo ndio makhsusi katika kuchunguza matumizi hayo ya dawa za kusisimua misuli.
Kikawaida ya mashindano yanapofanyika uwanja wa nyumbani basi mwenyeji ndiye anaepewa nafasi ya kutwaa ubingwa kutokana na kwamba anaungwa mkono na washabiki wengi, lakini kwa uhodari wa vijana wetu wa Zanzibar Heroes na kusua sua kwa timu ya taifa ya Kenya hio ilitoa kitisho kikubwa kwa Kenya kwamba huenda wakaangukia pua kwa mwaka huu.
Na hio ndio sababu kuu niionayo na niiaminiyo hadi kupelekea maafisa hao kuwatishia wachezaji wetu kuwatuhumu na baadae kuwagida mkojo sambamba na kuwanyonya damu kwa ajili ya vipimo vya dawa za kuengeza nguvu michezoni.
Kwa ulimwengu wa sasa wa sayansi, teknolojia na uwazi nilidhani matokeo yangetoka papo hapo, kwa ulimwengu wa sasa uliojaa uchu na uharaka wa mambo, sitaki niamini kama hakuna uwezekano wa matokeo ya vipimo hivyo kupatikana kabla ya mashindano hayo kuisha, ili kama kweli vijana wa 'Zanzibar Heroes' wanatumia madawa hayo yakuengeza nguvu wasiendelee kudhulumu timu nyengine kwa matokeo ya masaada 'kharam mutlaq' wa madawa hayo.
Na hapa ndipo pale ninapoamini kwamba zile zilikuwa ni hujma, njama na kuwajaza khofu sambamba na kuwatoa katika morali ya kuendelea kufanya vyema katika hatua zilizobakia, na hii naamini imekuja baada ya 'Zanzibar Heroes' kutoa salamu kwa timu ambazo walikuwa hawajacheza nazo.
Hivyo niwanasihi wachezaji wetu, Seleembe, Hilika, Feitoto, Banka na kikosi kizima, msikhofishwe na wala msitetereke, kwa sababu mimi siamini na wala sina uhakika kwamba dunia ya leo eti kipimo kisubiriwe miezi sita ndipo majibu yapatikane, kama maabara ya 'WADA' kwa ukanda wa Afrika yako Afrika ya Kusini, jambo la kujiuliza, kutoka Kenya kwenda Afrika ya Kusini ni masaa mangapi na kurudi masaa mangapi? jiengeze ikesha nipe jawabu hala uamini kama kweli maafisa wale waliku 'Serious' katika kulinda vitendo vichafu vya wanamichezo katika mashindano.
Bila shaka jawabu lako litakuwa kama ninavyoamini mimi, ikiwa ni hivyo basi pia amini kwamba hakuna majibu ya vipimo hivyo yatakayotolewa, cha muhimu nawaambia vijana waondoe khofu na wasiwasi watuletee kile tulichowatuma.
Makala hii imedukuliwa kutoka ukuta wa facebook uitwao Zanzibar Heroes 4 Zanzibaris na imeandikwa na:
Ali Mohammed (Almar)
Ali Mohammed (Almar)
Zanzibar.
Maoni
Chapisha Maoni