WAKALI SITA WA 'ZANZIBAR HEROES' WATATAWALA MECHI YA JANG'OMBE BOYS VS JKU JUMAMOSI, YUMO RAIS, SANGULA, FEI TOTO, MWALALA, WAWESHA NA PWINA

Katika mwendelezo wa ligi kuu visiwani Zanzibar kanda ya Unguja siku ya Jumamosi ya tarehe 23/12/2017, kutakuwa na mchezo wa ligi hio kati ya timu ya Jang'ombe Boys na JKU ambao ni mapingwa watetezi wa ligi hio, mchezo huo utavurumishwa katika dimba la uwanja wa Amani Zanzibar majira ya saa nane mchana (8.00).

mchezo huo ni wa kukamilisha mzunguko wa tisa (9th Round) wa ligi hio, ambao awali ulipangwa kuchezwa siku ya Jumatano ya tarehe 29/11/2017, lakini ulilazimika kusogezwa mbele kutokana na timu ya JKU kuingiza wachezaji wanne (4) katika timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) ambayo ilikuwa katika mashindano ya CECAFA yaliyomalizika nchini Kenya ambapo Zanzibar imeibuka nafasi ya pili katika mashindano hayo.


Mfungaji wa magoli yote mawili dhidi ya Kenya 
Khamis Mussa Makame (Rais) kutoka Jang'ombe Boys

Kitendo hicho cha kuwemo kwa wachezaji wanne wa JKU katika timu ya taifa ya Zanzibar, kanuni ya kuongozea ligi kuu Zanzibar inairuhusu timu yenye wachezaji kuanzia watatu katika timu ya taifa kuomba kupanguliwa ratiba yake hadi pale wachezaji wake hao watakaporudi katika vilabu vyao.

Katika mchezo huo wa Jumamosi tutashuhudia wakali wa Zanzibar Heroes wa vilabu vyote viwili yaani Jang'ombe Boys na JKU, ambao waliokuwa pamoja kwa kipindi cha zaidi ya wiki 2 wakilala pamoja, wakila pamoja wakiwa na mipango mimoja na wakiitumikia timu moja sasa wataanza kutofautiana katika dimba kwa kucheza vilabu tafauti.


Feisal Salum (Fey Toto) akifanya yake katika mchezo 
kati ya Taifa Stars na Zanzibar, ambapo Zanzibar ilishinda 2-1

Kwa upande wa JKU tutamuona kipa mahiri ambaye alifanya vizuri katika mashindano hayo Mohammed Abrahman (Wawesha), ambaye kama si umahiri na uhodari wake aliouonyesha katika mashindano hayo basi Zanzibar isingefika hatua hata ya kucheza nusu fainali.

Pia tutamuona beki kisiki mwenye nguvu na akili nyingi Issa Haidar Dau (Mwalala), ikumbukwe Mwalala alifanya kazi kubwa katika michezo yote ya CECAFA, ambapo bila kazi yake ya kijasiri akishirikiana na wenzake, ile dhana ya Zanzibar walaurojo ingesadifu.
Ibrahim Mohammed (Sangula) akikabana koo 
na mshambuliajiwa Rwanda ambapo Zanzibar ilishinda 3-1

Mwengine ni Amour Suleiman (Pwina), na yeye alitokea mechi ya Libya pekee na badae akaumia mazoezini, lakini Pwina naye ni mchezaji mzuri na anatarajiwa kuemo katika kikosi cha JKU dhidi ya Jang'ombe Boys Jumamosi.

Na wa mwisho ni kijana mdogo sana katika kikosi cha Zanzibar Heroes, kiungo khatari sana ambaye aliibuka mchezaji bora katika mchezo dhidi ya wenyeji Kenya katika mashindano hayo ya CECAFA, na baadae kuzua mjadala ya kwamba huenda yeye na wenzake wanatumia madawa ya kuengeza nguvu na baadae kuchukuliwa vipimo.

Kwa upande wetu Jang'ombe Boys, tulitoa wachezaji wawili pekee, ambao na wao hawakuwa lelemama bali wamekuwa roho ya Zanzibar Heroes na tegemeo kubwa la Wazanzibar na Kocha Hemed Suleiman (Morocco), hivyo na wao watatofautia na wenzao waliokuwa wakiitetea Zanzibar Heroes na sasa wataitetea Jang'ombe Boys kufa kupona.

Ibrahim Mohammed (Sangula) huyu ni nahodha wa timu yetu Jang'ombe Boys, ambaye kule Kenya akitumika kama mlinzi wa kulia tafauti na katika timu yeke ambapo anatumika kama beki wa kati, Sangula mwanzo hakupewa nafasi ya kufanya vizuri katika timu ya Taifa kwa nafasi hio ya beki wa kulia, lakini aliudhihirishia umma kwa vitendo kwamba ile msema wa kiswahili usemao "Mchagua jembe si mkulima" sote ni mashahidi ni jinsi gani aliitumikia namba hiyo kwake ngeni, aliitumikia utadhani ndiyo aliyozaliwa nayo.

Khamis Mussa Makame, hapa nakosa neno la kumuelezea huyu jamaa, kwa sababu ameondoka Jang'ombe Boys kwenda Zanzibar Heroes akiwa tayari na majina kadhaa tofauti na aliyozaliwa nayo kutokana na umahiri wake wa kuliona na kulijuwa goli la timu pinzani, ingawa jina hilo halikutumiwa na watangazaji wa Kenya kutokana na kutojulikana sana anga za nchio, sisi huyu tunamwita 'Rais' au 'Trump', baada ya kitendo chake cha kikatili kwa timu ya Kenya kufunga goli la kusawazisha dakika ambazo Wakenya na hadhara zote zilizoihudhuria mechi ile kiwanjani au luningani (TV) wakidhani kwamba ndio mpira umemalizika,  ndipo Rais akatumbukiza goli la kisanii na baadae kuipeleka mechi dakika za nyongeza Kenya wakafunga tena Rais akachomoa tena kisanii na kuipeleka mechi katika hatua ya penalti.

Vitendo vyote hivyo vimemfanya Rais kupewa majina lukuki, wengine kwa sasa wanamwita Mkombozi wa Zanzibar, Shujaa wa Zanzibar, lulu ya Zanzibar, almasi ya Zanzibar na mjina kedekede ambayo kila mmoja huita kutokana na hisia zake za kitendo hicho cha kiungwana kwa nchi yake.

Hivyo fika kiwanjani Amani saa 8.00 kamili mchana Jumamosi ya tarehe 23/12/2017 panapomajaaliwa ushuhudie wachezaji wa timu moja ya Zanzibar Heroes wakicheza timu tofauti, sambamba na kuthibitisha makali yao.

Fika mapema kwani kuna khatari ya mafuriko kuliko yale ya mapokezi.

SHARE NA MWENZAKO KUINUWA SOKA LA ZANZIBAR

Maoni