JOTO LA HOMA YA MECHI YA JANG'OMBE 'DABI' (DARBY) KATI YA JANGOMBE BOYS NA TAIFA YA JANG'OMBE LAPANDA MARADUFU.


Licha timu zote mbili Jang’ombe Boys na Taifa ya Jang’ombe kuondokewa na wachazaji wake mahiri katika vikosi vilivyowahi kukutana, lakini kila timu imeingiza wachezaji wengine wapya wenye hadhi za kuchezea timu hizo na kuleta furaha katika vilabu vyao, jambo ambalo washabiki wa timu hizo hutambiana pindi wanapokutana kwa usajili ambao vilabu vyao wameufanya.
Na: Ali Mohammed (Almar)
Kufuatia usajili huo uliomalizika na baadae wasimaizi na waongozaji mpira Zanzibar FA kutangaza mchezo huo wa upinzani kufanyika tarehe 18/01/2018, Jee! Taifa ya Jang'ombe watalivua ‘JINAMIZI’ la kufungwa na Jang’ombe Boys mfululizo katika msimu uliopita? Au Jang'ombe boys wataitandika tena Taifa ya Jang'ombe kwa mara ya nyengine na hatimae Taifa kuendelea kuwa mateja kwa Jang'ombe boys kama washabiki wa Jang’ombe Boys wanavyoamini?


Kwa mtaa wa Jang’ombe na viunga vyake tayari mtaa huo umeshaingia katika mchezo, homa zimeshatanda katika maskani na barza za vilabu hivyo, majikambo, tambo na majibizano ya hapa na pale ndio yamesheheni midomoni mwa wadau wa timu hizo huku kila upande ukijivunia ushindi kutokana na uwezo wa wachezaji wake.

Kama uliwahi kuukosa mchezo huu basi nikwambie kwamba hakika mechi hii si ya kukosa, kwani Jang'ombe Boys malengo yao ni yale yale, wana malengo mawili katika mchezo huo, kwanza kuendelea kuwatoa Taifa ya Jang'ombe maungoni sambamba na kuutambulisha umma wa wapenda soka kwamba wao ndio "Top in Jang'ombe".

Pili, ni kukwea katika nafasi za juu kupitia mgongo wa watani wao hao kama walivyofanya katika michezo ya ligi kuu 2016/17 kwa kuwafunga Taifa mfululizo, matokeo ambayo yaliifanya Jang'ombe Boys kuongoza ligi kabla ya Jamuhuri kuchukuwa uongozi wa ligi hio na baadae JKU waliupoka uongozi na JKU kuwa mabingwa.

Kwa upande wa Taifa ya Jangombe wao pia wana malengo mawili katika mchezo huo, moja, ni kuhakikisha wanaondoa uteja kwa majirani zao hao, kwani tayari wameshafungwa Mara mara nyingi kitendo ambacho kinawanyima raha,na pili, ni kuanza ukurasa mpya wa ushindi katika ligi hii ya 2017/18 kwa kuwafunga majirani zao hao na kuondoa ule uteja uliozoeleka mbele ya Jang’ombe Boys.

Kwa sababu hizo basi usikose kufika kiwanja cha Amani Stadium Siku ya Alhamis ya tarehe 18/01/2018 saa 10.00 alaasiri panapo uhai na majaaliwa, kushuhudia 'Jang'ombe Darby'.

HIZI HAPA RIKODI USO KWA USO BOYS V/S TAIFA WALIZOKUTANA
Timu hizI zimeshakutana mara 8 katika historia huku mara 5 Boys akishinda, mara 2 kafungwa na mara 1 sare ambapo Dabi hiyo ya Jang’ombe kati ya Taifa ya Jang’ombe na Jang’ombe Boys ndio dabi inayoongoza kwa kuhudhuriwa na watu wengi katika uwanja wa Aman na mji mzima wa Zanzibar huwa na minong’ono mingi kabla na baada ya mchezo huo.

Msimu wa mwaka 2016-2017 walikutana Novemba 19, 2016 katika Bonanza la Coconut FM ambapo matokeo Taifa 2-0 Boys mabao ya Taifa yalifungwa na Mkongo Baraka Ushindi na Mkenya Mohd Said “Mess ambaye kwa sasa hayumo katika kikosi cha Taifa.

Disemba 10, 2016 walikutana tena kwenye Ligi kuu soka ya Zanzibar Mzunguko wa kwanza na mataokeo Taifa 2-2 Boys ambapo mabao ya Taifa siku hiyo alifunga Omar Yussuf Chande aliyetimkia klabu ya Malindi dakika 9 na Abdallah Mudhihir (Mido) ambaye amerudi kikosini kutokea Singida United dakika 60 wakati mabao ya Boys yote alifunga Khamis Mussa (Rais) dakika ya 45 na 53 ambaye ndiye Shujaa wa Zanzibar aliyeifungia Zanzibar Heroes katika fainali ya CECAFA dhidi ya Kenya kule Machakos.

Disemba 30, 2016 pia walikutana tena kwenye Kombe la Mapinduzi 2017 na matokeo Taifa 1-0 Boys kwa bao pekee lililofungwa na Hassan Seif “Banda” ambaye kwa sasa ni mchezaji wa Jang’ombe Boys.
Aprli 25, 2017 walikutana tena kwenye ligi kuu soka ya Zanzibar Mzunguko wa pili na matokeo Taifa 0-1 Boys kwa bao pekee limefungwa na Khamis Mussa “Rais”.

Mei 14, 2017 walikutana tena kwenye ligi kuu soka ya Zanzibar hatua ya 8 bora Mzunguko wa kwanza na matokeo Taifa 0-3 Boys ambapo mabao ya Boys yalifungwa na Khamis Mussa “Rais”, Khatib Ng’ombe alijifunga mwenyewe na Juma Mess la tatu.

Na Jumapili ya Julai 30, 2017 kwenye mzunguko wa pili ligi kuu soka ya Zanzibar hatua ya 8 bora walikutana ambapo Boys alishinda 2-0 kwa mabao ya Hafidh Barik (Fii) aliyehamia Zimamoto kwa sasa dakika ya 6 na Juma Ali (Mess) dakika ya 66.

Msimu wa Mwaka 2012-2013 Boys aliwafunga Taifa mara mbili wakati huo timu zote zipo ligi Daraja la Pili Wilaya ya Mjini baada ya Boys kushinda 2-1 kwenye ligi hiyo, na mchezo mwengine Kombe la Waamuzi Boys tena kupata ushindi baada kushinda kwa penalti 5-4 kufuatia dakika 90 kumalizika kwa sare ya 0-0 michezo yote hiyo ilisukumwa katika Uwanja wa Mao Tsi Tung.

USIPITWE.

LikeShow More Reactions
Comment
Comments

Maoni