KUELEKEA MECHI NA TAIFA YA JANG'OMBE KOCHA SAID KWIMBI ASISITIZA UMOJA NA MSHIKAMANO


Kocha mkuu wa Jang'ombe Boys Said Omar 'Kwimbi' asisitiza umoja na mshikamano miongoni mwa wadau wa Jang'ombe Boys, akizungumza baada ya mazoezi ya timu hio mbele ya wachezaji, viongozi na wadau wa Jang'ombe Boys kocha Kwimbi amesema bila ya wadau wote wa timu kuwa pamoja kwa kila hatua basi ushindi hautapatikana.




"Tunakwenda kucheza mchezo wa ligi kuu na Taifa ya Jang'ombe siku ya Alhamis ya tarehe 18/01/2018, mchezo ambao unatambulika Zanzibar nzima na baadhi ya maeneo ya Tanzania, mchezo huo ni 'Dabi' yaani anaeshinda hapo ndiye bwana wa mtaa wa Jang'ombe.

"Niseme bila mashirikiano kuanzia viongozi, wanachama/washabiki, wachezaji na sisi walimu sote kuwa kitu kimoja, basi hakuna ushindi katika mchezo huo wala mwengine wowote, katika mchezo wa mpira wadau wote wanatakiwa kuwa kitu kimoja, na kila mdau atekeleze wajibu wake.

"Sisi makocha tutekeleze majukumu yetu, wachezaji watekeleze majukumu yao, viongozi watekeleze wajukumu yao, wanachama, watekeleze majukumu yao na mwengine yeyote mwenye mnasaba na timu hii atekeleze majukumu yake, endapo mmoja tu katika wadau niliowataja akitegea kutekeleza majukumu yake basi hakuna ushindi utakaopatikana.

"Hivyo niseme kuepuka kulaumiana, kutukanana kama wanavyofanya wenzetu basi ni wajibu wetu makundi haya ya wadau niliyoyaorodhesha tuwe kitu kimoja kwa kila hali, tukikosea tukae pamoja tuulizane wapi tulipokosea ili turekebishe natuache kutupiana lawama, lawama ambazo hazitatengeneza. Alimalizia Kocha Kwimbi.

Kocha Kwimbi hajawahi kusimamia mchezo kati ya Jang'ombe Boys na Taifa akiwa kama kocha, hivyo huo utakuwa ndio mchezo wa mwanzo kwa kocha Saidi Omar (Kwimbi) tangu ajiunge na timu hio.

Maoni