Jang'ombe boys leo itajitupa tena kiwanjani Amani 'Stadium' majira ya saa kumi za alasiri (10.00) kupambana na timu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (Kipanga SC), mchezo huo ni wa ligi kuu ya Zanzibar kanda ya unguja.
Katibu Friends of J.Boys, Alawi H. Foum
Kufuatia mchezo huo, Marafiki wa Jang'ombe Boys FC (Friends of J. Boys) wameendelea na kawaida yao ya kutoa zawadi kwa kila mchezo wa ligi kuu, ili kuwapa hamasa wachezaji wa timu hio katika suala zima la kupambana na kuiletea timu ushindi.
Akizungumza na mtandao huu katibu wa 'Friends of J.Boys' ndugu Alawi Haidar amesema kwamba wao kama marafiki wa timu yao, mbali ya kuwa na majukumu mengi ya timu lakini hili wameliona lina umuhimu sana katika maendeleo ya timu.
"Friends of J. Boys' ilianzishwa msimu uliopita na matunda yake tumeyaona katika msimu huo huo ulioanzishwa, hivyo huu ni muendelezo wetu wa kawaida, pamoja na kuonekana na wadau kwamba ni jambo la kawaida lakini kwa wachezaji wetu wanathamini sana utaratibu huu na kila mchezaji anatamani na yeye ifike siku aingie katika watu wanaozawadiwa na 'Friends of J. Boys'.
"Kitu kizuri wachezaji wote wanajuwa uwepo wa chombo hichi na zawadi tunazotoa hatuangalii 'Alphabet' za majina yao, hapana wanajuwa kwamba ili uzawadiwe basi lazima ufanye kazi katika mechi, aidha ufunge goli au uwonyeshe uwezo mkubwa wa uchezaji wenye kuisadia timu na hatimae uchaguliwe kuwa mchezaji bora.
"Hivyo nasisitiza kwa wachezaji kwamba, "Friends of J. Boys' tutaendelea kutoa zawadi katika mchezo huu dhidi ya Kipanga, zawadi zitakazotolewa ni kwa wachezaji wafuatao:
- Wafungaji wa Magoli hata yawe magoli 100, lakini timu iwe imeshinda, hatutatoa zawadi kwa kufungwa wala kutoa sare.
- Mchezaji Bora, na hapa mchezaji bora atachaguliwa endapo timu itashinda tu, timu ikifungwa au ikitoa sare hakutakuwa na zawadi.
"Pia tunazungumza na baadhi ya makampuni rafiki zetu watukubalie kutupa udhamini wa tunzo za uchezaji bora wa kila mwezi, tuko katika hatua nzuri mara tukishakuafikiana, basi tutawajulisha wadau na wachezaji ili wajuwe kuanzia mwezi gani zoezi hili litaanza" alimaliza katibu Alawi.
Mtandao huu haukuishia hapo ulitaka kujuwa ni zawadi gani zitakazotolewa, na kama ni fedha ni kiasi gani kitatolewa kwa wachezaji watakaofunga magoli na kiasi gani kitatolewa kwa mchezaji bora wa mechi na zawadi nyenginezo, mtunza hazina (mshika fedha) Ali Mohammed alikuwa na haya:
"Kama alivyosema katibu, ni kweli zawadi zitakazotolewa kwa mchezo wa leo, nazo ni kwa mchanganuo ufuatao kwanza ni cheti maalum kwa mchezaji bora ambacho kitasainiwa na katibu wetu, zawadi ya pili ni fedha taslim kwa mchezaji atakaekuwa bora kushinda wote (mchezaji bora wa mechi), zawadi ya tatu ni fedha taslim kwa wachezaji wote watakaofunga magoli, zawadi ya nne ni fedha taslim kwa mchezaji atakaefunga magoli matatu (hat-trick), zawadi ya tano ni mchezaji atakaefunga goli kwa kichwa, na zawadi ya sita ni mchezaji atakaefunga goli kwa shuti la nje ya 18.
"Kwa sasa sitaweka wazi ni kiasi kwa kila kitendo kitazawadiwa hadi hapo kamati yetu tendaji itakapokaa, kuamua na kupitisha hilo, isipokuwa nawaomba wachezaji na wadau wote watuamini kwani tumeshafanya mengi hapo mwanzoni hivyo waamini na hili pia litafanyika kwa uwezo wa Allah, na zawadi zote hizo zitatolewa siku ya pili katika kiwanja chetu cha mazoezi" alimalizia Mshika Fedha ndugu Ali Mohammed.
Mtandao huu unawasisitiza wachezaji kufanya vyema na kujituma katika mchezo wa leo ili kujinyakulia zawadi hizo sambamba na kuiletea ushindi timu yao, pia tunawakumbusha washabiki wetu kufika kwa wingi ili kuzidisha hamasa kwa wachezaji wetu.
Maoni
Chapisha Maoni