PAMOJA NA SULUHU YA 1-1 LAKINI VIJANA WANASTAHIKI PONGEZI

Kabla ya mchezo wengi ambao si marafiki zetu waliichukulia Jang'ombe Boys kuwa itafungwa na KMKM, ndio maana hata mahudhurio kiwanjani yaliongezeka kidogo, hata wale waliokuwa hawajaonekana siku nyingi kiwanjani walivutika kuja kiwanjani kushuhudia mchezo huu ambao kiupande fulani ulikuwa na ladha ya aina yake.

Na: Ali Mohammed.

Walifika kiwanjani kuja kuthibitisha mawazo yao hayo huku sisi tukiamini kwamba tutawafunga KMKM na kwa aliyekuepo kiwanjani kabla ya mchezo huo kuisha waliungana na sisi, na hata wale waliokuja kuthibitisha mawazo yao ya kwamba Jangombe Boys itafungwa na KMKM nadhani hawakuwa na budi kuipenda na kuishabikia japo kimoyomoyo timu yetu, kutokana na jinsi vijana walivyowajibika na kuwanyanyasa na kuwahenya maafisa hao wa kupambana na kuzuia magendo (KMKM).




Dhana zao za kwamba Jang'ombe Boys itapoteza mchezo ule kwa maafisa wa KMKM ni kwa sababu zifuatazo:


  1. Kwa kipindi cha hivi karibuni baada ya dirisha dogo la usajili, timu ya KMKM ilitomea mkwa kufanya usajili wa wachezaji wenye uzoefu na ligi kuu na hatimae kuonekana kuimarika.
  2. Kupata matokeo mazuri kwa KMKM tangu walipomaliza usajili wa dirisha dogo.
  3. Mwenendo wa kutopata matokeo mazuri kwa Jang'ombe Boys kwa msimu huu wa 2017/18.
  4. KMKM kuchukuwa wachezaji watatu nyota kutoka Jang'ombe Boys ambao ni Chinga, Shomari na Mbungi.
  5. Usajili wa bei ndogo na wachezaji wasiomaarufu katika ligi kuu uliofanywa na Jang'ombe Boys sambamba na kuondokewa kwao na wachezaji wake tisa wa kikosi cha kwanza kutimkia vilabu vyengine.
Hizi zilikuwa ndizo sababu kuu za kuamini kwao kwamba eti Jang'ombe Boys, watafungwa na KMKM iliyoimarika, matokeo yake Vijana wetu kama si kukosa nafasi nyingi na za wazi kufunga mabao basi maafandi hao wangekiona cha mtema kuni.

Tulimiliki mpira kwa kiasi kikubwa kitendo kilichopelekea KMKM kufanya mabadiliko dakika za mwanzo za mchezo, harakati zetu zilihitaji dakika 10 pekee kuandika goli la kuongoza kupitia kwa Khamisa Mussa Rais aliukwamisha mpira nyavuni kwa pasi safi na makini kutoka kwa mshambuliaji mwenzake Muhamadi Soud, huku tukikosa magoli mengi na ya wazi vipindi vyote viwili, jambo ambalo kwa utamaduni wa kiafrika ingawa mimi siukubali sana ingawa mambo hayo yapo watu walihusisha na mambo ya kishirikina, eti KMKM wameroga kuyafanya magoli yasiingie, lakini mimi naamini bahati haikuwa yetu kwa siku ya jana.

Washambuliaji wetu wote walikosa magoli, Abdi Kassim Babi alikosa nafasi 3 nzuri, Khamis Mussa ingawa alifunga goli lakini alikosa nafasi si chini ya nne, Tafa alikosa nafasi mbili nzuri, Muhamadi Soud nafasi 6, ambapo 2 ndani ya box dogo, Khatibu mesi aliyeingia kipindi cha pili alikosa nafasi moja kwa kupiga shuti dhaifu iliyokamatwa na mlinda mlango kirahisi kabisa, huku wachezaji kama Rashid Muhammed (Chidi) kupiga mashuti fyongo na wengineo.

KMKM hawakupata nafasi nyinga na hata nafasi walizozipata hazikuwa za kutisha kutokana na ulinzi ulioimarika wa timu yetu ni nafasi moja pekee ya wazi iliyopatikana, ambayo mshambuliaji wetu wa zamani aliyehamia KMKM Abrahaman Othman (Chinga) aliukwamisha mpira wavuni na kuwafanya KMKM kushangilia na kupuuwa nyuso zao katika dakika za 87.

Hakuna lawama kwa mchezaji yeyote katika mchezo na suluhu ile kwa sababu kila mmoja alijituma na kutekeleza majukumu aliyopangiwa kwani hata tukisema watu wamekosa magoli mengi jawabu lake ni kwamba hakuna mchezaji anaengia kiwanjani akanuia leo nataka nikose magoli, kila mmoja ana lengo apate magoli ili timu ipate ushindi, isipokuwa mchezo wa mpira ni mchezo wa makosa na bahati, makosa hayaepukiki kwa binadamu yeyote lakini bahati inakosekana kwa kila binaadamu.

Hivyo kwa kuwa kila kitu kinakwenda kwa bahati, basi tuamini waliokosa magoli hawakuwa na bahati na waliopata ndio ilikuwa bahati yao, la muhimu ni kuwapongeza vijana kwa upambanaji wa hali ya juu, tuendelee kushikamana ili kutengeneza matokeo mema na yenye kupendeza kwa michezo inayofuata, kwa sababu ligi haijaishia kwa KMKM, ligi bado inaendelea.

Hongereni wachezaji wetu kwa kupambana na kuonyesha soka safi sana.

Maoni