JANG'OMBE BOYS WAKWEA KILIMANI KWA KISHINDO, YAILAZA KILIMANI CITY 3 - 1


Jang'ombe boys FC leo imefanikiwa kukwea kilimani kwa kishindo kikubwa baada ya kuifunga timu yenye majigambo, mipasho na tambo nyingi hususan katika mitandao ya kijamii Kilimani City yenye maskani yake katika magorofa ya Kilimani.


Ulikuwa ni mchezo mzuri na wa kuvutia mchezo ambao ulitawaliwa zaidi na Jang'ombe Boys kwa kutandaza soka safi lililojaa mbinu na ufundi wa hali ya juu, kitendo ambacho kilipelekea Jang'ombe Boys dakika ya 12 kuandika goli la kwanza kupitia kwa kiungo wake mshambuliaji Helfini Salum (Fini) aliyepokea pasi ya mahaba kutoka kwa mshambuliaji machachari Mustafa Vuai (Tafa).

Bila ya ajizi Fini aliukwamisha kimiani kwa kupiga shuti kali iliyompita kama umeme kipa hodari wa Kilimani City na kuifanya Jang'ombe Boys iongoze 1-0.

Jang'ombe Boys walikosa nafasi nyingi za kufunga kutokana na umakini mdogo wa washambuliaji wake, kitendo kilichopelekea mchezo huo kwenda mapumziko Jang'ombe Boys wakiwa wanaongoza kwa goli 1-0.

 Kilimani City wakionekana kuanza kwa kasi kidogo ili kujaribu kushomoa goli, lakini vijana wa Jang'ombe Boys walionekana kubadilika na kuumiliki mpira, ambapo dakika  ya 38 fundi Abdi Kassim Saadalla (Babi) akaiandikia Jang'ombe Boys bao la pili na kuyafanya matokeo huwa 2-0, lakini dakika 2 baadae Kilimani City wakasawazisha goli na kuyafanya matokeo kuwa 2-1.

Jang'ombe Boys hawakuridhika na matokeo hayo waliendelea kulisakama lango la Kilimani City na katika dakika za nyongeza baada ya dakika za kawaida kumalizika,  mshambuliaji mwenye nguvu, mbio, akili na ujasiri mkubwa Muhamadi Soud alimshinda beki kisiki wa Kilimani City ambaye ni raia wa Nigeria na kuwa piga chenga mabeki wengine wawili pamoja na kipa na kuiandikia Jang'ombe Boys bao la tatu, na hadi firimbi ya mwisho inapulizwa Jang'ombe Boys 3 Kilimani City 1.

Kikosi cha mwanzo cha Jang'ombe Boys:


  1. Hasham Haroun
  2. Mansour Marzouk
  3. Juma Ali
  4. Firdaus Seif
  5. Ibrahim Mohamed (C)
  6. Said Yussuf
  7. Mustafa Vuai
  8. Abdi Kassim
  9. Muhamadi Soud
  10. Khelfein Salum
  11. Rashid Mohammed.
Kikosi cha Kilimani City:
  1. Yussuf Abdi
  2. Innocent Njoku
  3. Idd Said
  4. Saad Mgeni
  5. Mohd Hussein
  6. John Elias
  7. Chande Abdalla
  8. Abdillahi Seif
  9. Humud Suleiman
  10. Zubeir Mkombozi
  11. Hassan Juma.

Maoni