Kabla ya siku ya leo
timu yetu imekuwa na wiki nzuri, wachezaji wamehudhuria vizuri mazoezini, wadau
na washabiki pia na wao walijitokeza kwa wingi kuipa hamasa na sapota ya
nguvu timu yao kila siku ya mazoezi, sambamba na kuonyesha mapenzi makubwa kwa
wachezaji wao.
Kama hio haitoshi
washabiki na wapenzi na viongozi na wao wamekuwa pamoja kujadili, kuzungumza na
kupanga kwa wiki nzima juu ya mchezo huu ambao umekuwa ukisubiriwa kwa hamu na
washabiki wa mpira wa miguu, ili kuona kwamba jee Charawe wataweza kuzima moto
ambao umewashwa na Jang'ombe Boys, moto ambao umetoa kitisho kwa timu zilizo
nafasi ya juu katika msimamo wa ligi kuu ya Zanzibar (ZPL) inayoendelea.
Charawe ambayo naweza
kusema tayari imekata tiketi ya kushuka daraja, imekuwa na kawaida hio ya
kuwasimamisha vigogo wa ligi kuu pindi wakikutana, ingawa mpira una matokeo
matatu yaani kufungwa, kushinda na kutoka suluhu, lakini kwa uimara wa
wachezaji na aina ya mazoezi sidhani kama Charawe wanaweza kutuzuia tusipate
matokeo muhimu joini ya leo.
Nini kinanipa matumaini
ya kwamba timu yetu itashinda katika mchezo wa leo?
UMOJA NA MSHIKAMANO WA
TIMU.
Taasisi zote
ulimwenguni, ili zifikie mafanikio ya malengo ni lazima angalau taasisi hio
nusu na robo ya wanaounda taasisi hio, lazima wawe wamoja na washikamane.
Kwa mnasaba huo hapo
tumefanikiwa kwa sababu katika timu yetu hatuna mgawanyiko wa aina yeyote,
viongozi, wachezaji, wanachama, washabiki na wadau wote wapo kitu kimoja kwa
lengo moja tu, nalo ni kuhakikisha mechi inakwenda vizuri na mafanikio, kitu
ambacho kinanipa moya na imani kubwa ya ushindi.
MATAYARISHO MAZURI YA
MCHEZO.
Tulikuwa na muda mrefu
wa kujiandaa na mchezo huu baada ya kumaliza mchezo uliopita kwa mafanikio pale
tulipoifunga Kilimani City 3-1, hivyo wadau wote kwa uwezo wao wametimiza
wajibu wao kwa timu yao ili kujiandaa na mchezo huu ili kuupata ushindi wa timu
yao.
UZIMA WA WACHEZAJI.
Tunamshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kuwaponya wachezaji wetu wale waliokuwa wanaumwa, kwa sasa kikosi
kimeimarika, Hassan Seif 'Banda' amerudi kutoka kuuguza bega lake, hivyo niseme
kurudi kwa Banda kutaengeza chachu ya ushindi kwani kumekuwa na ushindani wa
hali ya juu katika mazoezi kwa washambuliaji wetu watatu, nakusudia Banda, Muhamadi
na Rais.
AINA YA MAZOEZI.
Hii ndio faida ya kuwa
na mchezaji mwenye uzoefu wa muda mrefu na aliyepitia vilabu vingi kwa sababu
ukisajili mchezaji kama huyo, huwa umesajili kocha mchezaji, maana huwa wana
vitu vya ziada, kinachotakiwa ni utayari tu wa wachezaji na timu yenyewe.
Kwa sasa nampongeza sana
mchezaji wetu mkongwe Abdi Kassim 'Babi', kiukweli anachokifanya sasa ndipo
mahali pake hasa, kwa mfumo wa mazoezi anayoyaongoza Abdi kwa washambuliaji na
viungo wetu, hakika hakuna timu itayoweza kuzuwia moto wetu.
Ukiangalia moto
tuliwasha katika michezo iliyopita, kosa letu kubwa lilikuwa ni kutengeneza
nafasi tumemiliki mpira mechi zote zilizopita lakini tumetengeneza nafasi
chache na tatizo jengine ni kutia magoli, uwezo wetu umekuwa si zaidi ya magoli
mawili licha ya kumiliki mpira kwa kiwango kikubwa, lakini kwa mfumo huu ambao
'Babi' kwa kushirikiana na Kocha Amasha, nadhani hakuna wa kutusimamisha
kuanzia sasa tukianza na mchezo wa leo.
HITIMISHO.
Kwa mnasaba huo basi
sina shaka na mchezo wa leo kwamba utakuwa ni wenye kutubeba, na hautatubeba
bure bure bali ni kutokana na juhudi zetu, kuanzia wachezaji kwa kuhudhuria
mazoezi kama kawaida na kuwa wazima wa afya, wadau na washabiki kwa jitihada
zao za kihali na kimali, nasaha na mawazo yao chanya kwa viongozi wao, viongozi
kwa kuwa wamoja na wasikivu kwa wanayoshauriwa, walimu kwa kuwanasihi,
kuwafunza sambamba na kuwasahihisha wachezaji makosa yao pamoja na dua njema
kutoka kwetu na walio upande wetu.
Muhimu zaidi tufike
mapema na kwa wingi sana ili tuishangirie timu yetu kwa umoja wetu na kwa nyoyo
zetu.
Jang'ombe Boys ni yetu
sote.
Mungu Ibariki Jang'ombe
Boys FC - AMIIN.
Maoni
Chapisha Maoni