KOCHA AMASHA ASISITIZA WACHEZAJI KUENDELEA NA UMAKINI KATIKA TIMU

Kocha wa Jang'ombe Boys Issa Othman Ali 'Amasha' amewataka wachezaji wake kutobweteka na matokeo mazuri wanayoyapata wachezaji wake, kocha Amasha ameyasema hayo baada ya kumalizika kwa mchezo wa jana wa ligi kuu dhidi ya Charawe FC ambapo timu yake iliibuka na ushindi wa goli 2-0.



Amasha akiwa mbele ya wachezaji wake amesema, "Ndugu zangu katika mashindano yeyote hasa hasa mchezo wa mpira wa miguu, kila mechi moja ngumu inapomalizika ndipo mechi nyengine ngumu zaidi inapokuja, nasema hivi kwa kuwa nilisema tangu tuko mazoezini kwamba tunakwenda kucheza na timu moja ngumu sana kwa wakati huu, na hatimae wenyewe mmeshuhudia ugumu wake.

"Hivyo niseme ushindi na mengine iliyopita iwe ndio chachu ya kutaka kushinda zaidi ili tufikie malengo, hivyo hakuna kubweteka na matokeo, hakuna kuvimbisha vichwa, najuwa watu watawasifu sana sasa hivi lakini ukisifiwa wewe itikia ahsante lakini katika kichwa chako sema mimi bado na kuonyesha kwamba kweli wewe bado basi ni kuhakikisha kila mmoja anahudhuria mazoezi kwa wakati na anafanya bidii katika mazoezi.

"Nafahamu kila mmoja ana malengo mazuri katika mpira, ili malengo ya mpira yawe upande wako, basi siri kubwa ni kutokata tamaa na kufanya mazoezi kwa dhati ya moyo sambamba na kupendana miongoni mwenu nyinyi wachezaji" Alimalizia Amasha.

Baada ya mazungumzo hayo Kocha Amasha alitangaza mapumziko ya siku moja, hivyo mazoezi yataendelea tena mnamo siku ya Jumatano ya tarehe 28 Machi 2018 ili kujinoa na timu ya Zimamoto.

Maoni