DAKIKA 2.37 ZATOSHA KUVUNJA MAULIDI YA WATOTO WA CHUONI

Naam, hakuna marefu yasio na mwisho, hakuna rekodi isiyovunjwa, bali ni umri, siku na saa.


Hatimae timu yetu imevunja mwiko wa kutoifunga timu ya Chuoni FC, mwanzoni historia baina ya timu hizo ilionyesha kwamba, Chuoni FC walinekana ndio wenye kuongoza kuweka rekodi ya kuifunga J.Boys almaarufu "Wastaarabu wa Ng'ambu".

Lakini katika mchezo wa leo uliofanyika katika kiwanja cha Amani saa 10 alasiri, zilihitajika dakika 2 na sekunde 37 pekee kuibadili historia hio, baada ya mshambuliaji mwenye nguvu nyingi, mwenye mbio nyingi, mwenye akili nyingi na mwenye mashuti ya nguvu Muhamadi Soud kupokea pasi safi kutoka kwa Frank 'Telela' katikati ya uwanja na kuwakimbia mabeki wa Chuoni FC na kuachia shuti kali mithili ya umweso lililokwenda moja kwa moja wavuni.

Hilo ni goli la kwanza kwa mshambuliaji huyo katika ligi kuu ya Zanzibar tangu kusajiliwa wakati wa usajili wa dirisha dogo akitokea timu ya Good hope ya Mkwajuni Kaskazini mwa kisiwa cha Unguja,  Muhamadi ameshacheza michezo mitano ya ligi kuu bila ya kuifungia timu yake hio, lakini ameshafunga magoli 6 katika mechi 4 za majaribio wakati wa harakati za usajili wake.

Chuoni walipata nafasi ya kubadilisha matokeo hayo, lakini shukurani zimwendee golikipa Hasham Haroun Ruga kwa kufanya kazi yake inavyotakiwa na kwa ushujaa wa hali ya juu.

Hivyo kwa matokeo hayo sasa Jang'ombe Boys inapaa hadi nafasi ya sita katika msimamo wa ligi kuu ya Zanzibar. Kwa mujibu wa kocha Issa Othman, timu itaendela na mazoezi hapo kesho tarehe 14/03/2018 na tarehe 16/03/2018 timu itashuka tena dimbani kuchuana na timu ya Kilimani City.

kikosi cha Jang'ombe Boys FC kilichoanza ni:

Hasham Haroun
Mansour Marzouk
Juma Mohammed
Firdaus Seif
Ibrahim Mohammed
Said Kitarabu
Mustafa
Abdi Kassim
Frank 'Telela'
Helfeni Salum
Muhammad Soud


Maoni