HUKU 'RAIS' HAPA 'MAKAMO' HAWAWEZI KUZUIA MOTO USIWAKE

"Huku 'Rais' hapa 'Makamo' hawawezi kuzuia moto usiwake", haya ndio maneno yaliyosheheni katika vinywa vya washabiki wa Jang'ombe Boys, wakimaanisha kwamba kwa uwezo wa washambuliaji walionao basi hakika Zimamoto kufungwa ndio hukumu yao.

Washambuliaji pacha wa Jang'ombe Boys, 
Muhamadi Soud (Makamo) na Khamis Mussa (Rais)

Ni ukweli usiopingika kwamba kwa sasa timu ya Jang'ombe Boys ndio timu yenye washambuliaji hatari na wenye kutisha, unapomzungumzia 'Rais' hapa anakusudiwa  mshambuliaji wetu Khamis Mussa, ambaye kwa wapenzi wa mpira wa miguu Afrika Mashariki, kati na kusini yake anajulikana vya kutosha kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuzifumania nyavu sambamba na kuwahenyesha walinzi wa timu pinzani.

Hivyo kwa uwezo huo unaotambulika huwezi kuwashangaa washabiki wa Jang'ombe Boys ukiwakuta wanajitamba na timu yao na uwezo wao kupambana, kwani ili timu ipate ushindi lazima iwe na washambuliaji wanaolijuwa goli la timu pinzani, na kwa mshambuliaji kama Khamis Mussa amelithibitisha hilo mara nyingi katika historia yake ya soka, hasa hasa tukirudia matukio katika fainali za Chalenj kule Kenya.

Kwa upande mwengine, kwa siku za karibuni tangu usajili wa dirisha dogo ukamilike, utawasikia washabiki wa Jang'ombe Boys wakitaja jina la 'Makamo wa Rais', Makamo wa rais hapa anakusudiwa mshambuliaji pacha wa Khamis Mussa, si mwengine bali ni Muhammad Soud, kijana mdogo ambaye ana miaka 21 pekee,  aliyeibuliwa kutoka kijiji cha Mkwajuni kaskazini mwa kisiwa cha Unguja, huyu ni kijana mwenye mambo mengi sana licha ya kuwa mwanagenzi katika ligi kuu na hata mazingira ya mjini.

Pamoja na ugeni wake wa mji na Ligi kuu, lakini tayari ameanza kuonyesha uwezo wake mkubwa katika safu ya ushambuliaji na ufungaji, amekuwa akitoa pasi za magoli sambamba na kufunga magoli safi, na maogli mengine hutumia juhudi binafsi kufunga magoli yake, hivyo ukiwasikia washabiki wa Jang'ombe Boys wakijisifia kuhusu mshambuliaji huyu, basi kubaliana nao kwamba wana kila haki na ruhusa ya kujisifia.

Sasa kwa muktadha huo basi ule msemo wao wa "Huku 'Rais' hapa 'makamo' hawawezi kuzuia moto usiwake" kwa kiasi kikubwa unaweza kusadifu katika mchezo wa ligi kuu kati ya Jang'ombe Boys dhidi ya Zimamoto hapo kesho panapomajaaliwa, ambapo timu hii  ya Zimamoto inatokana na Jeshi lenye dhamana ya kuzima moto na kuzuia maafa, ambapo historia inaonyesha kwamba timu hizi zinapokutana huwa ni patashika nguo kuchanika.

Lakini kwa kikosi cha Jang'ombe Boys kilichopo sasa, kilichosheheni kila aina ya vipaji, kilicho katika morali ya juu ya kutaka kupata mafanikio katika msimu huu, bila shaka Zimamoto hawataweza kuzuia moto utakaowashwa na Jang'ombe Boys wala hawataweza kujinusuru wao wenyewe na maafa yaliyo mbele yao dhidi yetu.

Sisi ni 'Wastaarabu wa Ng'ambu' tutahakikisha tunaeneza ustaarabu kila kona kupitia mpira wa miguu.

Maoni