JANG'OMBE BOYS MABINGWA KOMBE LA MUUNGANO

Ni dhahiri kwamba vijana wetu wako sawa na wanauwezo wa kupambana katika sehemu yeyote, uwanja wowote, nchi yeyote na mazingira yeyote.

Hili wamelithibitisha hapo jana tarehe 26/04/2018 katika kiwanja cha Bandari jijini Dar es salaam baada ya kuibuka kidedea mbele ya timu ya Karume market na kukabidhiwa kombe pamoja na zawadi 'kemkem', mchezo huo ulikuwa ni wa fainali, ambapo fainali hio inaashiria kwamba lile kombe la Muungano ambalo lililosimama kwa miaka mingi sasa limezinduliwa rasmi.



Mchezo ulianza kwa kasi huku timu ya Karume Market ambayo msimu ujao wa 2018/19 itacheza ligi kuu ya Vodacom Tanzania wakimiliki mpira zaidi kitendo ambacho kiliipelekea timu hio kuandika goli la kuongoza mnamo dakika ya 5 ya kipindi cha kwanza.

Timu zilikwenda mapumziko matokeo yakiwa tuko nyuma kwa goli moja bila ya majibu, lakini baada ya msahihisho kutoka kwa waalimu Jang'ombe Boys walionekana kubadilika na kuchukuwa hatamu ya kumiliki mpira huku wakigongeana pasi na kufanya mashambulizi ya mipango, kitendo kilichowafanya mashuhuda wa mtanange huo kuanza kuishangilia Jang'ombe boys kwa kandanda safi wanalolionyesha.

Kwenye dakika ya 70, mshambuliaji Muhamadi Soud akiwa katika harakati za kuukwamisha mpira wavuni, akiwa tayari ameshawapiga chenga mabeki wawili na akiwa tayari ameshamdanganya golikipa ndipo kiungo wa Karume Market aliyekuwa akirudi golini kujaribu kusaidia timu akamkwatua kwa nyuma mshambuliaji huyo ndani ya boksi (penalt box) na kuamuliwa penalti, penalti ambayo iliwekwa kimiani na Mustafa Vuai (Tafa) na kufanya matokeo kuwa 1-1.

Hadi dakika 90 zinamalizika Jang'ombe Boys 1-1 Karume Market, hapo ndipo mchezo ukaingia katika hatua ya matuta, ambapo katika penalti tano za mwanzi Jang'ombe Boys walipata penalti nne, penati moja Suleiman Ali (Pichori) alikosa na Karume Market wakakosa penalti moja.

Katika penalti za nyongeza Jang'ombe Boys walipata penalti mbili na Karume Market wakapata moja na kukosa penalti moja, kitendo ambacho ndicho kilichoipa timu yetu ushindi wa penalti 6-5 na kutawazwa kuwa mapingwa wa mashindano hayo.

Timu ya Jang'ombe boys itawasili katika bandari ya Malindi majira ya saa nane na nusu za mchana wa leo, mnaombwa kujitokeza kwa wingi ili kuipokea timu yetu.

Hongereni vijana zidisheni kasi na bidii ili kuipa heshma timu yetu ndani na nje ya Zanzibar.

Maoni