LAITI TUNGEWAPATA KATIKA KIWANJA BORA, TUNGEMALIZA MCHEZO DAKIKA ZA MAPEMA: MAKAMO WA RAIS

Mshambuliaji machachari wa Jang'ombe Boys Muhamadi Soud (Makamo wa Rais), amesema kama mechi ingechezwa katika kiwanja chenye ubora zaidi ya waliochezea, basi dakika 45 tu zingetosha kuumaliza mchezo huo kwa kuwafunga wapinzani wao timu ya Karume Market magoli zaidi ya matatu.





Muhamadi Soud ameyasema hayo akiwa nyumbani kwake katika kijiji cha Mkwajuni Kaskazini ya Unguja wakati mtandao huu ulipotaka kujuwa tathimini ya mchezo huo kutoka kwake, ikiwa ni mechi yake ya kwanza kuichezea timu hio nje ya Zanzibar.

"Nimefurahia mazingira ya safari, mazingira ya hoteli ambayo tumefikia, mazingira rafiki ya timu yetu. ila kitu kimoja pekee ndicho sikukifurahia, ambacho ni uwanja tuliochezea, haukuwa na ubora sana wa kuchezea mechi kubwa kama ile.

"Laiti kama tungewapata katika kiwanja kilicho bora zaidi ya kile tulichochezea, basi tusingefika hatua za matuta, tungemaliza mchezo ndani ya dakika 45 za mwanzo, kwa sababu tulikuwa bora, tuliwakamata kila idara, mpaka mashabiki wao wakafurahishwa na timu yetu.

"Kitu pekee nashukuru kwamba nimecheza mchezo wangu wa kwanza nje ya Zanzibar nikiwa na kiwango bora, niliwasumbuwa sana, hadi wakawa wananipiga na hdi goli letu la kusawazisha ni kutokana na usumbufu wangu" alisema Muhamadi Soud.

Jang'ombe Boys wameifunga Karume Market kwa penalti 6-5 baada ya kwenda suluhu ya 1-1 katika dakika 90, na matokeo hayo yakaifanya Jang'ombe Boys kuwa mabingwa wa kwanza wa kombe la Muungano ambalo limezinduliwa rasmi mwaka huu, hivyo hii ni historia mpya na ya muhimu sana kwetu.




Maoni