NAHODHA 'SANGULA' AITAKA MECHI DHIDI YA ZIMAMOTO

Nahodha wa Jang'ombe Boys Ibrahim Mohammed (Sangula) amesema licha ya kutoonekana katika mazoezi na timu yake kwa kipindi takriban siku 10, amesema yuko fiti na anahamu kucheza mchezo wa ligi kuu utakaochezwa siku ya Ijumaa ya tarehe 06/04/2018 katika kiwanja cha Amani.


Ibrahim Mohammed (Sangula)


Akizungumza kwa njia ya simu na mtandao huu, Sangula amesema amelazimika kutokuwa katika mazoezi na timu kwa kipindi chote hicho, hii ni kutokana na mambo ya kifamilia ambayo yamemlazimu kusafiri kwenda Tanzania bara ili kuweka sawa mambo hayo ambayo hakupenda kuyaweka wazi.

"Mimi kwa sasa niko huku Tanzania Bara ambapo hata uongozi wangu unatambua hilo, kwa sababu niliondoka kwa kuomba ruhusa na nashukuru nilipatiwa ruhusa hio ingawa siku nilizopewa mwanzo zilikwisha, lakini kwa kuwa mawasiliano yapo huwa nawasiliana na uongozi ili kutoa taarifa kwamba bado mambo hayajakaa sawa na uongozi unanielewa.

"Hivyo nitarudi Zanzibar kesho Alhamis (leo) kwa boti ya asubuhi au mchana ili niungane na timu yangu, na niko fiti kwa sababu huku niliko nafanya mazoezi kama kawaida, kwa sababu mimi ni mchezaji ninaejielewa popote ninapokwenda nasafiri na vifaa vyangu vya mazoezi ili niweze kuuweka mwili vizuri katika hali ya utayari, hivyo hakutakuwa na tofauti katika uchezaji wangu, naamini mambo yatakuwa mazuri tu.

"Niseme bado mambo yangu ya kifamilia niliyoyafata huku bado hayajamalizika, lakini kwa sababu naipenda timu yangu na naujuwa ugumu wa mchezo wetu na Zimamoto pindi tunapokutana, ndio maana nikaona nisiiache timu yangu bila ya uwepo wangu, hivyo endapo mwalimu akiona kuna haja ya mimi kucheza katika mchezo huo basi niko tayari kuitikia na kuitumikia timu yangu ili tukae pazuri katika msimamo wa ligi. alimalizia Sangula.

Mchezo wa Ijumaa dhidi ya Zimamoto ni miongoni mwa michezo muhimu sana kutokea katika timu yetu, kutokana na kwamba endapo tukifanikiwa kuibuka washindi katika mchezo huo basi tutaondoka nafasi ya tano ambayo tupo sasa na tutakwea hadi nafasi ya 3 katika msimamo, hivyo kuna haja kila mdau kuungana na timu kwa hali na mali kuisaidia timu ili ifanikiwe malengo yaliyopangwa.


Maoni