RASMI JANG'OMBE BOYS KUFUNGUA MASHINDANO YA KOMBE LA FA KANDA YA UNGUJA

Tetesi tetesi zilizokuwa zikizungumzwa takriban miezi minne nyuma sasa zathibika, tetesi hizo zilikuwa ni juu ya suala zima la uanzishwaji wa kombe la FA kwa upande Unguja, ambapo timu 64 zitashiriki mashindano hayo ambayo ni mashindano ya mtoano (knockout), hayo yameelezwa leo na Katibu wa Jang'ombe Boys Abdalla Mahfoudh (Dallas) wakati akizungumza na mdandao huu.

Katibu wa Jang'ombe Boys Abdallah Mahfoudh aliye katikati
akitekeleza majukumu yake.

"Kwanza sina budi kuwashukuru wadau wote wa timu, kuanzia wachezaji ambao wao ndio sura ya timu, wanachama na washabiki ambao wao ndio roho ya timu, viongozi wote ambao wao kwangu mimi ndio kichwa cha timu, shukrani hizi ni maalum kwa uungaji mkono wao kwa hali na mali katika msimu wa ligi kanda ya Unguja ambapo timu yetu ilishiriki na kufanikiwa kumaliza katika nafasi ambayo tumeibakisha timu yetu katika ligi kuu, kwani wapo wenzetu waliotamani wafike hapa tulipofika sisi, lakini bahati haikuwa yao.

"Jengine ambalo ndilo ninalotaka kuliarifu kwa hadhira ya soka Zanzibar pamoja na wadau wetu Jang'ombe Boys ni kwamba, katika kile kilichokuwa kikizungumzwa miezi iliyopita ya kwamba huenda kwa mara ya kwanza Zanzibar kutaanzishwa FA cup, hatimae hili jambo kweli limeanzishwa na ni jambo la kushukuriwa sana, kwa sababu kila nchi duniani inayo mashindano kama haya na huwa ni mashindano yenye hadhi kubwa, bila shaka waandaaji watayapa hadhi inayofanana na wenzetu kwa hali zetu.

"Hivyo katika uteuzi wa timu uliofanywa, na sisi tumebahatika kuwemo katika mashindano hayo, mbali ya uteuzi huo pia tumepewa heshima ya kwamba sisi ndio wafunguaji wa pazia la mashindano hayo, heshima ambayo ni historia na fakhari ya timu yetu kwa sisi tuliopo sasa na kwa warithi wetu, kwani hili halitafutika, ambapo kila miaka ikisonga ikizungumzwa historia ya kombe hili Zanzibar basi lazima Jang'ombe boys itajwe na itambuliwe kwa uasisi wake huo.

"Mashindano haya yatazishirikisha timu 32 kutoka madaraja mbali mbali, ambapo yatakuwa katika mtindo wa 'Knockout' maana yake atakaefungwa atakuwa ameyaaga mashindano hayo na atakaeshinda atasubiria ratiba ya 16 bora ambayo itatolewa baada ya hatua ya awali kukamilika, hivyo sisi tutaingia katika kiwanja cha Amani siku ya Jumamosi ya tarehe 23/06/2018 saa 10.00 alaasiri kufaana na timu ya Dulla Boys" alisema katibu.


Pia katibu Dallas hakuacha kuwaomba wadau hao wa Jang'ombe Boys kurudi katika mstari ambao ulivunjika kwa muda kupisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, ili kuweka historia ya kulibeba kombe hilo ambalo limeasisiwa kwa ushauri wa Dkt. Ali Mohamed Shein.

"Kwa maana hio basi kuna haja ya wadau wote wa timu warudi katika msatari, kama ilivyo kawaida yetu, tushikamane, tuungane na tukamatane ili tueke historia nyengine ya kuchukuwa vikombe vinavyoasisiwa kama tulivyofanya katika kombe la Muungano.

"Kwa kuwa naamini mtandao wetu huu unasomwa na watu wengi, sina shaka taarifa hii itawafika wote wadau na wapenda soka wote wa Zanzibar ili walitambue jambo hili" alisisitiza Dallas.

Akijibu suala aliloulizwa na mtandao iwapo kwa upande wa Pemba nako mashindano hayo yatakuepo kama ilivyo kwa upande wa Unguja, Katibu Dallas amesema zipo taarifa kwamba Pemba wao walishaanza na wako katika hatua za mwishoni kabisa.

".....Kwa upande wa Pemba, wao inasemekana wakati ligi kuu ilipokuwa ikiendelea michezo hii ya FA pia ilikuwa ikichezwa, hii ni kutokana wao afadhali wana viwanja vingi vinavyoruhusu kuchezewa mashindano, na kwa sasa mashindano hayo ya FA kwa pemba yapo katika hatua za mwishoni" Alimalizia Dallas.





Maoni